Papa Francis atoa wito wa kuvumiliana Misri

Papa Francis
Image caption Papa Francis

Papa Francis ameongoza misa iliyohudhuriwa na maelfu ya waumini wa kanisa katoliki katika mji mkuu wa Misri Cairo.

Waumini walikongamana kwenye uwanja, ambapo walipeperusha bendera na kuachilia puto zilizokuwa na rangi za Vatican wakati papa akiingia.

Ziara yake inajiri wakati ambapo kumekuwa na mauji ya Wakristo wengi katika mashambulizi, na katika hotuba yake, papa Francis ametoa wito wa kuvumiliana.

Ibada hiyo ilifanyika katika uwanja wa wanajeshi, na iliongozwa kwa lugha ya Kiarabu na Kilatino.

Aliwarai viongozi wa dini zote kukemea uhalifu wowote unaotekelezwa kwa misingi ya kidini.

Jana Papa Francis alizuru kanisa moja mjini Cairo Misri ambapo takriban Wakristo 30 waliuawa katika shambulio lililotekelezwa na wapiganaji wa Islamic State mwezi Disemba mwaka jana.

Aliandamana na kiongozi wa kanisa la Coptic nchini humo, Pope Tawadros.