Eminem ashtaki chama tawala cha New Zealand

Wimbo wa Lose Yourself wake Eminem ulitumiwa katika filamu yake ya 8 Mile Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Wimbo wa Lose Yourself wake Eminem ulitumiwa katika filamu yake ya 8 Mile

Mwanamuziki mashuhuri Eminem amekishtaki chama tawala cha New Zealand kuhusiana na wimbo wake ambao umetumiwa kwenye tangazo la kampeni.

Rapa huyo amesema wimbo uliotumiwa katika tangazo la chama cha National Party mwaka 2014 ulikuwa makala ambayo haikuwa imeidhinishwa ya wimbo wake wa Lose Yourself.

Lakini mawakili wa chama hicho wanasema wimbo uliotumiwa haukuwa wa Lose Yourself, bali ni wimbo ufahamikao kama Eminem-esque ambao waliununua kupitia soko la jumla la muziki mtandaoni.

Kesi hiyo ilianza Jumatatu, ambapo nyimbo zote mbili zilichezwa katika ukumbi wa mahakama.

Wakili wa Eight Mile Style, kampuni inayomuwakilisha mwanamuziki huyo, amesema wimbo wa Lose Yourself ulikuwa na kipekee na bila shaka ni fahari ya kazi za sanaa za Eminem.

Tangazo hilo la mwaka 2014 lilikuwa na picha za wapiga makasia na sauti nyuma yake ikiwahimiza watu kudumisha "timu ambayo inafanya kazi" na kurejesha National Party madarakani katika uchaguzi uliokuwa unakaribia.

Wimbo uliotumiwa, Eminem-esque, unakaribiana sana na Lose Yourself, ambayo ulitumiwa katika filamu ya Eminem ya 8 Mile ambayo ilitolewa 2002.

Wimbo huo ulitolewa kwa hazina ya nyimbo zilizoandaliwa na kampuni ya Beatbox.

Haki miliki ya picha NATIONAL PARTY
Image caption Tangazo la chama cha National Party cha New Zealand

Nyimbo ambazo hukaribiana sana na nyimbo halisi ambazo ni maarufu sana, lakini zina tofauti kidogo vya kutosha kutokiuka sheria ya hakimiliki, mara kwa mara huwekwa kwenye masoko ya pamoja ya nyimbo zilizo huru kutumiwa.

Lakini wakili wa Eight Mile Style Gary Williams amesema matumizi ya wimbo huo ulikuwa ni ukiukaji wa sheria ya hakimiliki.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii