Donald Trump amwalika Duterte ikulu ya White House

Trump aliwasiliana na Duterte kwa njia ya simu Haki miliki ya picha EPA
Image caption Trump aliwasiliana na Duterte kwa njia ya simu

Rais wa Ufilipino Rodrigo Duterte amepewa mwaliko kwenda White House baada ya kuwa na mawasiliano "ya kufana" kwa njia ya simu na Rais Donald Trump.

Viongozi hao wawili walishauriana kuhusu vita tata vya Duterte vya kukabiliana na mihadarati, ambavyo vimesababisha kuuawa kwa watu karibu 7,000 katika kipindi cha miezi 12.

Mzozo kuhusu Korea Kaskazini pia ulijadiliwa.

Kwa mujibu wa White House, Bw Trump alifurahia sana mazungumzo hayo, na alitoa mwaliko, ingawa tarehe yenyewe ya ziara hiyo haikuafikiwa.

Ziara hiyo itakuwa fursa ya "kujadiliana kuhusu umuhimu wa ushirikiano wa Marekani na Ufilipino, ambao kwa sasa unaendelea kuimarika," taarifa ya White House ilisema.

Mkutano kati ya Bw Duterte na Barack Obama mwaka uliopita ulifutiliwa mbali baada ya Duterte kumuita Obama "mwana wa kahaba".

Bw Duterte ameshutumiwa vikali na jamii ya kimataifa kutokana na ukatili wake katika kukabiliana na walanguzi na watumizi wa dawa za kulevya nchini Ufilipino.

Maelfu ya washukiwa wa ulanguzi wa dawa wameuawa na polisi au makundi ya watu wenye silaha.

Maelfu wengine wamekamatwa.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Bw Trump amesema alifurahishwa na mawasiliano yake na Duterte

Rais huyo, ambaye sawa na Bw trump, alichaguliwa kuwa rais mwaka jana, pia amesema anaweza kufurahia sana kuua mamilioni ya waraibu wa dawa za kulevya nchini humo.

Bw Trump mwenyewe ni mtu ambaye amekuwa akitoa matamshi ya kutatanisha.

Aliwaita wahamiaji wa Mexico nchini Marekani kuwa "wabakaji".

Amekuwa pia akitumia maneno ya kudhalilisha kuwarejelea wanawake.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii