Mzee wa Indonesia aliyedai alikuwa na miaka 146 afariki

Mbah Ghoto (babu Ghoto), alizaliwa Desemba 1870 Haki miliki ya picha EPA
Image caption Mbah Ghoto (babu Ghoto), alisema alizaliwa Desemba 1870

Raia wa Indonesia ambaye alidai kwamba alikuwa na umri wa miaka 146 - binadamu aliyeishi muda mrefu zaidi duniani - amefariki dunia kijijini mwake Java ya Kati.

Kwa mujibu wa stakabadhi alizokuwa nazo, Sodimedjo, aliyefahamika pia kama Mbah Ghoto (babu Ghoto), alizaliwa Desemba 1870.

Lakini Indonesia ilianza kunakili rasmi visa vya watu kuzaliwa mwaka 1900, na kumewahi kutokea makosa awali.

Hata hivyo, maafisa waliambia BBC kwamba nyaraka na stakabadhi alizokuwa nazo zilikuwa halali.

"Tunaamini stakabadhi hizi ni halali, kwa mujibu wa nyaraka rasmi za serikali. Tunaamini tarehe yake ya kuzaliwa ni sahihi," anasema afisa wa serikali Wahyu Wiyanto.

Alipelekwa hospitalini mnamo 12 Aprili baada ya afya yake kudorora.

Siku sita baadaye, alisisitiza kwamba aruhusiwe kurejea nyumbani mwake.

"Tangu arudi kutoka hospitalini, alikunywa vijiko vichache tu vya uji na kunywa maji kidogo," mjukuu wake Suyanto ameambia BBC.

"Yalidumu siku chache tu. Kuanzia wakati huo hadi kifo chake, alikataa kula na kunywa."

Siri ya maisha marefu?

Alipoulizwa siri ya maisha yake marefu, Mbah Ghoto aliambia BBC mwaka jana kwamba siri yake ni kuwa "nina watu wanaonipenda na wanaonitunza."

Alikuwa anavuta sigara sana hadi mwisho wa maisha yake.

Aliishi muda mrefu kuwashinda wake zake wanne, ndugu zake 10 na watoto wake wote.

Haki miliki ya picha FAJAR SODIQ

Mbah Gotho alichukuliwa kama shujaa eneo analotoka.

"Siku ya Uhuru alikuwa akialikwa kusimulia yaliyotokea wakati wa vita. Anaweza kusimulia kuhusu vita dhidi ya wakoloni kutoka Japan na Uholanzi," anasema Wahyu Wiyanto.

Mjukuu wake alisema awali kwamba mzee huyo alikuwa hana masharti mengi na alikuwa haitishi chakula maalum.

"Kitu pekee alitutaka tufanye ni kununua jiwe la kaburi lake," anasema.

Mzee huyo alisema mwaka jana kwamba alikuwa anaishiwa na nguvu na hakutarajia aishi muda mrefu zaidi.

"Sina nguvu kama zamani. Hata kutembea ni shida. Nilikuwa mkulima na nilivua samaki mtoni. Sitaki kuendelea kuishi sana, ndio maana nimeandaa kaburi. "Ili nikifariki, kila kitu kiwe tayari," alisema.

"Kwa sasa nataka tu kufariki, lakini wakati wangu haujafika bado."

Mjukuu wake alisema babu yake alizikwa Jumatatu asubuhi katika makaburi ambayo aliyanunua miaka michache iliyopita.

Jiwe la kaburi ambalo alinunua mapema, na ambalo lilikuwa limekaa nje ya nyumba yake kwa miaka mingi, liliwekwa juu ya kaburi hilo.

"Hakuitisha mengi. Kabla afariki, alitutaka sisi, jamaa zake, tumwache aende," mjukuu wake alisema.

Huwezi kusikiliza tena
Mbah Ghoto alivukuwa mvutaji sigara sugu

Mtu ambaye aliishi miaka mingi zaidi duniani kulingana na Guinness ni Jeanne Calment kutoka Ufaransa ambaye aliishi miaka 122 na siku 164 .

Aliaga dunia mwezi Agosti mwaka 1997.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii