Donald Trump: Ningependa kukutana na Kim Jong-un

Kim na Trump Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Trump alisema Jumapili kwamba Kim Jong-un ni mtu mwerevu

Rais wa Marekani Donald Trump amesema angependa kukutana na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un, iwapo kungekuwa na mazingira mahsusi.

Amesema ingekuwa "heshima kuu kwake".

"Kungelikuwa na hali mahsusi kwangu kukutana naye, ningekutana naye - bila shaka. Ingekuwa heshima kuu kwangu kufanya hivyo," Bw Trump aliambia shirika la habari la Bloomberg Jumatano.

Jumapili, alikuwa amemweleza Bw Kim kama "kijana mwerevu".

Tamko la Bw Trump limetokea huku wasiwasi ukiendelea kuongezeka kuhusu mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini.

Ikulu ya White House baadaye ilitoa taarifa kufafanua matamshi ya Bw Trump na kusema Korea Kaskazini ingehitaji kutimisha masharti mengi kabla ya mkutano kati ya viongozi hao wawili kufanyika.

Msemaji wa ikulu hiyo Sean Spicer alisema Washington inataka kuona tabia ya uchokozi ya Korea Kaskazini ikikoma mara moja.

"Ni wazi kwamba kwa sasa, hakuna mazingira mahsusi (ya kufanikisha mkutano kama huo)," aliongeza.

Kwenye mahojiano na CBS Jumapili, Rais Trump alisema Bw Kim alichukua mamlaka akiwa na umri mdogo, licha ya kukabiliana na "watu wagumu na hatari sana."

Alisema hajui iwapo Bw Kim ana akili timamu.

Kiongozi huyo wa Korea Kaskazini aliamrisha mjomba wake auawe miaka miwili baada yake kuingia madarakani.

Aidha, anatuhumiwa kuamuru kuuawa kwa ndugu wake wa kambo.

Rais Trump, alipoulizwa maoni yake kuhusu kiongozi huyo wa Korea Kaskazini, aliambia CBS: "Watu wanajiuliza: 'Je, ana akili timamu?' Sijui mimi...lakini alikuwa kijana wa miaka 26 au 27...pale babake alipofariki dunia. Bila shaka amekuwa akikabiliana na watu wakali na wagumu, hasa majenerali wa taifa hilo na wengine.

"Na akiwa an umri mdogo hiyo, aliweza kudhibiti madaraka. Watu wengi, nina uhakika, walijaribu kumpokonya madaraka, iwe mjomba wake au watu wengine. Na alifanikiwa kuchukua na kuyadhibiti madaraka hayo. Kwa hivyo, bila shaka, ni kijana mwerevu."

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kim Jong-un, akizuru shamba la kufugia nguruwe. Kim ameapa kuendelea kufanyia majaribio makombora

Jumamosi, Korea Kaskazini ilifanya jaribio la kurusha kombora la masafa marefu ambalo lilifeli, mara ya pili kwa jaribio kama hilo kutekelezwa na Pyongyang katika kipindi cha wiki mbili.

Hali ya wasiwasi imekuwa ikiongezeka siku za karibuni, huku Korea Kaskazini na Kusini zikifanya amzoezi ya kijeshi.

Marekani imetuma meli za kivita na nyambizi eneo hilo na pia imeweka mtambo wa kutungua makombora ya adui Korea Kusini, mtambo ambao maafisa wanasema umeanza kufanya kazi.

Jumapili, makala katika shirika la habari la serikali ya Korea Kusini KCNA ilitoa wito kwa Marekani kutafakari kuhusu "madhara makubwa ambayo yanaweza kusababisha na uchokozi wake wa kipumbavu wa kijeshi."

Korea Kaskazini imekuwa ikifanya majaribio ya makombora mara kwa mara miezi ya karibu na imekuwa ikitishia kufanya jaribio la silaha za nyuklia kwa mara ya sita.

Rais Trump aliambia CBS kuwa Marekani "haitakuwa na furaha sana" iwapo majaribio zaidi yatatekelezwa na Korea Kaskazini.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Ndege ya kijasusi ya Marekani ikitua Korea Kusini

Alipoulizwa iwapo hili litasababisha hatua ya kijeshi kutoka kwa Marekani, alijibu: "Sijui mimi. Naam, tusubiri tuone."

Image caption Uwezo wa makombora ya Korea Kaskazini

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii