Wanasayansi wafanikiwa kufumua jeni za mchai

Huwa kuna ladha sita kuu za chai Haki miliki ya picha LIZHI GAO
Image caption Huwa kuna ladha sita kuu za chai

Wataalamu wa mimea nchini China wamesema wamefanikiwa kufumua na kufahamu zaidi kuhusu jeni za mchai.

Utafiti huo kuhusu mea huo ambao kitaalamu hufahamika kama Camellia sinensis, umewawezesha kupata ufahamu zaidi kuhusu jinsi chai inavyopata ladha yake.

Kufikia sasa, wanasayansi walifahamu mambo machache sana kuhusu muumbo wa jeni za mmea huo, licha ya umuhimu wake mkubwa kitamaduni na kiuchumi duniani.

"Kuna ladha nyingi tofauti za chai, lakini siri kuu ni: Nini huamua au nini huchangia ladha hizi mbalimbali za chai?" mtaalamu wa jeni za mimea Lizhi Gao wa taasisi ya Kunming Institute of Botany, China, aliyeongoza utafiti huo amesema.

"Pamoja na muundo wa ramani ya jeni hizi pamoja na teknolojia ya kufahamu mpangilio wa jeni, tunajaribu kuandaa chembe za jeni za mchai za kutusaidia kuchunguza baadhi ya ladha yake."

Kundi la mimea ya Camellia, huwa na jumla ya mimea 100, mingi ambayo ni mimea ya maua. Lakini ni Camellia Sinensis pekee ambao hukuzwa kibiashara kwa ajili ya kuzalisha chai.

Haki miliki ya picha YONG SHENG YI
Image caption Mwanasayansi akichuma majani ya kufanyiwa utafiti

Watafiti hao wamegundua kwamba majani ya mchai huwa na viwango vya juu sana vya kemikali zinazoipa chai ladha yake.

Kemikali hizi ni pamoja na flavonoids na caffeine.

Mimea mingine ya kundi la Camellia huwa na kemikali hizi lakini kwa viwango vya chini.

Dkt Monique Simmonds, naibu mkurugenzi wa sayansi katika Kew Royal Botanic Gardens, Uingereza ambaye hakushriiki katika utafiti huo anasema matokeo hayo ni muhimu sana katika kutoa maelezo kuhsuu chembe zinazounda jeni za chai.

Amesema itasaidia sana wote wanaohusika katika kuzalisha aina tofauti za chai na pia mimea inayotumiwa kuandaa manukato na bidhaa za urembo.

Kufumua chembe zinazounda jeni za mchai ni shughuli iliyowachukua watafiti hao miaka mitano.

Chembe za jeni za mchai zinakadiriwa kuwa na chembe pacha za DNA za urefu wa bilioni tatu, ni ndefu zaidi ya mara nne ukilinganisha na chembe za jeni za mmea wa kahawa.

Chembe hizo ni ndefu kuliko mimea mingi ambayo wataalamu wamefanikiwa kuzifumua.

Matokeo ya utafiti huo yanaweza kusaidia kuimarisha ubora wa chai na bei yake pia, kwa kuzalisha michai inayotoa majani chai ya hali ya juu zaidi.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii