Ndege ya kwanza kubwa ya kubeba abiria iliyotengenezewa China yapaa

C919 Haki miliki ya picha AFP

Ndege kubwa ya kwanza ya kubeba abiria ambayo imeundiwa nchini China imekamilisha safari yake ya kwanza.

Ndege hiyo imeundwa kutoa ushindani kwa ndege zinaozundwa na Boeing ya Marekani na Airbus ya Ufaransa.

Ndege hiyo ilikaa angani kwa dakika 90 kisha ikarejea salama katika uwanja wa ndege wa Pudong mjini Shanghai.

Hatua hiyo ni dhihirisho ya ndoto kuu ya China kutaka kuwa na ushindani katika sekta ya uchukuzi wa angani duniani.

Ndege hiyo inamilikiwa na shirika la ndege ya serikali ya Uchina, Comac. Safari ya ndege hiyo imekuwa ikipangiwa kufanyika tangu 2008 lakini hilo limekuwa likiahirishwa mara kwa mara.

Katika safari hiyo ya Ijumaa, ndege hiyo iliwabeba watu wachache sana. Ilikuwa na marubani watano pamoja na wahandisi, na maelfu ya wageni waheshimiwa walikuwa wamefika kushuhudia ikipaa.

Kabla ya safari hiyo, runinga ya taifa ilikuwa imesema ndege hiyo ingepaa hadi mita 3,000 juu ya usawa wa bahari pekee (futi 9,800), mita 7,000 chini ya upeo ambao ndege kwa kawaida hupitia.

Ndege hiyo ilifikia kasi ya kilomita 300 kwa saa (maili 186).

Ndege hiyo iliyopewa jina C919 imeungwa kushindana moja kwa moja ya 737 ya Boeing na Airbus A320.

Inakadiriwa kwamba soko la uchukuzi wa ndege duniani litafikia thamani ya jumla ya $2tn (£1.55tn) katika miaka 20 ijayo.

Ndege hiyo ya China bado imetumia teknolojia kutoka nje ya nchi hiyo, mfano injini zake zilitoka kutoka kwa kampuni ya CFM International yenye viwanda Marekani na Ufaransa.

Maafisa wanasema wamepokea maombi zaidi ya 500 ya ununuzi wa ndege hizo, na wateja 23 tayari wamethibitisha kwamba wako tayari kuzinunua.

Haki miliki ya picha Getty Images

Kampuni nyingi zinazotaka kununua ndege hizo ni za China, kuu ikiwa China Eastern Airlines.

Mambo muhimu kuhusu C919

  • C919 ina njia moja ya kupitia abiria ndani yake.
  • Ina uwezo wa kubeba abiria 168.
  • Itakuwa na uwezo wa kusafiri kati ya kilomita 4,075 na 5,555km kwa wakati mmoja (maili 2,532 - 3,452).
  • Kwa mujibu wa vyombo vya habari China, bei yake itakuwa takriban $50m, karibu chini ya nusu ya bei ya Boeing 737 au Airbus A320.
Haki miliki ya picha AFP

Shirika linalosimamia usalama wa safari za ndege Ulaya imeanza utaratibu wa kutathmini na kuidhinisha ndege hiyo ya C919 - ambayo ni hatua muhimu kwa ndege hiyo, ndipo iweze kufanikiwa katika soko la kimataifa.

China imekuwa na ndoto ya kuwa na sekta yake ya uundaji wa ndege tangu miaka ya 1970 pale mke wa kiongozi wa wakati huo Mao Zedong, Jiang Qing, binafsi alipounga mkono mradi huo.

Lakini ndege ya Y-10, iliyoungwa mwishoni mwa miaka ya 1970 haikufanikiwa kutokana na uzito wake.

Ni ndege tatu za aina hiyo pekee ambazo ziliundwa.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii