Mapigano makali mpaka wa Afghanistan na Pakistan

Kuna taarifa kuwa pande zote mbili zimekuwa na maafa na majeraha Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kuna taarifa kuwa pande zote mbili zimekuwa na maafa na majeraha

Wanajeshi kutoka Afghanistan na Pakistan wanakabiliana vikali kwa risasi, mpakani mwa mataifa hayo mawili, hatua iliyosababisha Pakistan kufunga kituo chake cha mpakani cha Chaman.

Pakistan inasema kuwa polisi wa Afghanistan walioko mpakani, walianza kuwamiminia risasi wanajeshi waliokuwa wakiwalinda maafisa wa shughuli za kuwahesabu watu.

Kiongozi mkuu wa hospitali ya serikali huko Chaman, ameiambia BBC kuwa, yamkini watu 10 wameuawa na zaidi ya 30 wamejeruhiwa.

Afisa mmoja mkuu katika jimbo la Kandahar, anasema kikosi cha maafisa wa Pakistani walikuwa wakiendelea na zoezi la kuwahesabu raia mpakani.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Kituo cha mpakani cha Chaman, kaskazini mwa makao makuu ya jimbo hilo Quetta, kinatumika kama lango la kuingilia mji wa Kandahar, kusini mwa Afghanistan

Mataifa hayo mawili yanagawanywa na eneo dogo la mpakani, lililochorwa na Uingereza na kupingwa na Afghanistan.

Makabiliano makali yanashuhudiwa huko Luqman na Jahangir, vijiji vinavyogawanya mpaka huo.

Uhusiano kati ya mataifa hayo mawili unazidi kudorora kila uchao, huku nchi hizo zikilaumiana kwa kushindwa kudhibiti wanamgambo wa kivita wanoingia katika mataifa hayo.

Mapema mwaka huu, Pakistan ilifunga mpaka wake, baada ya kuongezeka kwa mashambulio ya mara kwa mara.