Watoto 30 wa shule wafariki katika ajali Tanzania

Watu wakijaribu kunusuru baadhi ya watoto waliohusika katika ajali ya basi nchini Tanzania Haki miliki ya picha The Citizen
Image caption Watu wakijaribu kunusuru baadhi ya watoto waliohusika katika ajali ya basi nchini Tanzania

Huzuni na hofu imetanda katika mji wa Karatu na Arusha nchini Tanzania mapema alfajiri kufuatia ajali mbaya ya barabarani ambayo imewaua takriban wanafunzi 30 pamoja na walimu wao.

Ajali hiyo ilitokea saa tatu alfajiri kulingana na ripoti za eneo hilo la ajali ambalo liko takriban kilomita 150 kutoka mji wa Arusha.

''Wanafunzi wengi wameuawa, naweza kuthibitisha idadi kamili'' ,alisema mkuu wa wilaya ya Karatu Theresea Mahongo ambaye alikuwa akiongea na The Citizen Tanzania muda mfupi baadaye.

Alisema kwamba alikuwa Arusha kikazi na kwamba alikuwa anaelekea katika eneo hilo baada ya kupokea habari za mkasa huo.

Ripoti kutoka kwa walioshuhudia na maafisa wa elimu kulingana na The Citizen zimesema kuwa kati ya wale waliofariki 28 walikuwa wanafunzi huku watatu wakiwa watu wazima pengine walimu wao.

Waliofariki walitoka katika shule ya Lucky Vincent EnglishMedium School iliopo Mrombo kusini magharibi mwa mji wa Arusha na walikuwa wanaelekea Karatu kufanya mtihani wa pamoja katika shule mshirika ya Karatu.

Ripoti zinasema kuwa basi hilo liliteleza na kukosa mwelekeo ,likatoka katika barabara na kuanguka katika mto katika eneo la Marera eneo la Rhotia, kilomita chache kabla ya karatu katika barabara ya Arusha.

Picha katika vyombo vya habari vya Tanzania zinaonyesha basi lililoanguka katika bonde huku watu wakijaribu kutoa miili na watu waliojeruhiwa katika basi hilo.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii