Kiongozi wa mgomo wa kutokula arekodiwa akila gerezani

Bwana Marwan Barghouti alirekodiwa akila biskuti kisiri tarehe 27 mwezi Aprili. Haki miliki ya picha EPA
Image caption Bwana Marwan Barghouti alirekodiwa akila biskuti kisiri tarehe 27 mwezi Aprili.

Idara ya magereza nchini Israel imetoa video inayodaiwa kuonyesha kiongozi wa mgomo wa wiki tatu unaofanywa na wafungwa wa kipalestina akila kwenye chumba chake.

Idara hiyo inasema kuwa Bwana Marwan Barghouti alirekodiwa akila biskuti kisiri tarehe 27 mwezi Aprili.

Idara hiyo haikusema ni kwa njia gani alipata chakula hicho lakini taarifa zikiliambia gazeti la Haaretz kuwa alikuwa ametegwa,.

Mkewe Barghouti alisema kuwa video hiyo ni bandia na ilinuia kuvunja moyo kwa wale wanaofanya mgomo huo wa kutokula.

Zaidi ya wafungwa 890 wamekuwa wakisusia chakula tangu tarehe 17 mwezi Aprili wakilalamikia mazingira mabaya kwenye magereza ya Israeli.

Wametoa orodha ya matakwa ikiwe huduma bora za afya, kutembelewa mara kwa mara na familia na kumalizika kufungwa bila kufunguliwa mashtaka.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Video hiyo ilitolewa wakati wafungwa wa kipalestina walimaliza mgomo wao wa kutokula wa wiki tatu