Kongamano la London litaifaa Somalia?

Al-Shabab wameendelea kutekeleza mashambulio ya kujitoa mhanga Mogadishu Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Al-Shabab wameendelea kutekeleza mashambulio ya kujitoa mhanga Mogadishu

Alhamisi hii, jamii ya kimataifa itakongamana jijini London, kujadili hatima ya taifa la Somalia, nchi ambayo imekuwa ikiongoza katika orodha ya mataifa Hafifu kwa miaka minane kati ya 10 iliyopita.

Kongamano la London kuhusu Somalia, ambalo litaongozwa na Uingereza, Somalia na Umoja wa mataifa, litafanyika katika Jumba la Lancaster katika mtaa wa St James's. Wengi wa wajumbe watakaa katika hoteli za kifahari zilizoko hapo karibu.

Huu ndio mkutano wa tatu mkuu wa aina hiyo kufanyika London tangu 2012, na ajenda ni kama ni sawa - usalama, utawala bora na uchumi.

Stakabadhi rasmi za ratiba na mpangilio wa mkutano huo zinaashiria hatua kubwa ambazo zimepigwa na taifa hilo.

Lakini sifa za Somalia kama ilivyokuwa wakati wa mkutano wa kwanza zimebaki sawa: "taifa lisilo thabiti na ambalo halitawaliki", na linatishiwa na wanamgambo wa Kiislamu, uharamia na baa la njaa.

Lakini kunazo hatua chache zilizopigwa.

Uharamia, ambao wakati visa vilikuwa zimeongezeka zaidi ulikuwa unagharimu $7bn (£5.4bn) kwa maka, kwa sasa umepungua, ingawa karibuni visa vimeanza kuongezeka.

Marekani, kwa kutumia ndege zisizo na marubani, pamoja na wanajeshi wa kulinda amani wa Muungano wa Afrika, wanajeshi wa Somalia na washauri wa kiusalama kutoka nchi za Magharibi, wamefanikiwa kuwatimua al-Shabab kutoka kwenye miji mingi mikubwa.

Lakini wapiganaji hao bado wanadhibiti maeneo mengi na huwa wanatekeleza mashambulio mara kwa mara.

Rais mpya Farmajo

Uchaguzi ulifanyika hivi majuzi, na Mohamed Abdullahi Mohamed, maarufu kama Farmajo, akachaguliwa kuwa rais. Kuna pia wanawake wengi na vijana katika bunge la nchi hiyo.

Somalia ipo katika hali ya "kabla ya baa la njaa" badala ya kuwa katika janga kamili kama ilivyokuwa mwaka 2011, ambapo zaidi ya watu robo milioni walifariki dunia.

Na kwa njia ya kushangaza, ukame wa sasa hautakuwa miongoni mwa mambo makuu yatakayokuwa yanajadiliwa katika kongamano hilo.

Marekani yaipa Kenya ndege 6 za helikopta

Nchi hiyo inakabiliwa na ukame mbaya zaidi katika miongo kadha. Mvua imekosa kunyesha vyema kwa misimu minne mtawalia na Umoja wa Mataifa unasema watoto 275,000 watakabiliwa na utapiamlo ambao unatishia maisha yao mwaka 2017. Idadi ya watoto wanaokabiliwa na utapiamlo imeongezeka kwa asilimia 50 tangu mwanzo wa mwaka huu, na kufikia 1.4 milioni. Wengi ni wagonjwa sana kiasi kwamba hawawezi kwenda shuleni au kuchunga mifugo, jambo linalotishia maisha na uwezo wa wafugaji wa kuhamahama nchini humo.

Watu tayari wanafariki kutokana na njaa na maradhi ambayo huzidia watu kutokana na njaa. Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema kuliripotiwa zaidi ya visa vya 25,000 vya kipindupindu miezi minne ya kwanza 2017, na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka maradufu na kufikia 54,000 ifikapo mwezi Juni. Watu zaidi ya 500 wamefariki kutokana na ugonjwa huo.

Image caption Watoto ambao wameathiriwa na utapiamlo wakiwa hospitalini Baidoa

Watoto wanaokabiliwa na utapiamlo huwa hatarini ya kufariki kutokana na maradhi kama vile ukambi na ugonjwa wa kuharisha mara tisa zaidi ya watoto wasio na utapiamlo.

Si binadamu pekee wanaoumia. Katika eneo lililojitangazia uhuru wake la Somaliland, maafisa wanasema asilimia 80 ya mifugo wamefariki. Mifugo ndio tegemea la wengi. Mifugo walio hai husafirishwa nje ya nchi kuliko eneo jingine lolote duniani kupitia bandari za Somaliland na Djibouti,m hasa kuelekea Ghuba.

Hata kabla yako kuingia hospitali ya kanda ya Burao, katika eneo lililokabiliwa na njaa la Togdheer, Somaliland unaweza kusikia vilio vya watoto walioodhoofika kutokana na ukosefu wa chakula.

Mvulana mmoja, aliyevalia mavazi ya rangi ya zambarau anatazama ukuta. "Ubongo wake umeathirika kutokana na ukosefu wa chakula," Dkt Yusuf Ali, aliyerejea Somalia kutoka Uingereza miaka miwili iliyopita anasema.

"Hatapata nafuu kabisa."

Ukosefu wa usalama

Kusini magharibi mwa Somalia, maelfu ya watu walioathiriwa na ukame wametorokea Baidoa, ambapo wanaishi kwenye mahema viungani mwa mji huo. Eneo hilo liliathiriwa sana na ukame miaka ya 2011 na 1991. Eneo hilo hufahamika sana kama "pembe tatu ya mauti".

"Al-Shabab wanawachukua vijana wetu na wanaume ambao tuliwaacha nyuma, na kuwaahidi dola kadha za Marekani na chakula," anasema mwanamke mmoja.

"Bila hiari yao, watoto wetu na wanaume wamegeuzwa kuwa wapiganaji wapya wa kundi hilo."

"Tatizo kubwa katika kukabiliana na ukame huu ni ukosefu wa usalama," Sharif Hassan Sheikh Aden, rais wa jimbo la Kusini Magharibi, anasema akiwa Baidoa.

Jiji hili, ambalo hulindwa na wanajeshi wa Ethiopia, linapatikana katikati mwa ngome ya al-Shabab.

"Wapiganaji hawa wamefunga barabara zote, hivyo hatuwezi kufikisha chakula kwa wale wanaokihitaji."

Hili linaonesha ni kwa nini usalama ni suala kuu katika kongamano la sasa.

Somalia ikiendelea kutokuwa na usalama, itakuwa vigumu kufikisha misaada kwa wanaohitaji, sawa na maendeleo.

Image caption Maelfu ya watu wanaokimbia njaa na al-Shabaab wanaishi katika mahema viungani mwa Baidoa

Jimbo jipya la Kusini Magharibi ni moja ya majimbo ambayo yanajumuisha serikali mpya ya pamoja ya Somalia.

Wakosoaji hata hivyo wana wasiwasi kwamba kuundwa kwa majimbo hayo kutaigawa zaidi Somalia, na kuleta sura mpya kwa mapigano nchini humo.

Mwaka uliopita, kulitokea mapigano makali kati ya majimbo ya Puntland na Galmudug.

Mtazamo wa watu wa jimbo la Kusini Magharibi unaonesha jinsi mfumo wa serikali moja ya taifa na majimbo ulivyo.

"Tumetengwa kwa muda mrefu na kudunishwa na Wasomali wengine,2 anasema Fatima Issa, ambaye ni mkulima.

"Wafugaji huwadunisha wakulima."

"Hatuna wanajeshi wa serikali ya taifa hapa. Huwa hawawawindi al-Shabaab jinsi wanamgambo wetu hapa hufanya. Tunafaa kupigania uhuru zaidi, au hata tujitenge na kujitangazia uhuru wetu, kama walivyofanya Somaliland mwaka 1991."

Moja ya malengo ya Kongamano la London ni kufanikisha ufanisi zaidi na ugawanaji wa rasilimali kati ya majimbo na serikali ya taifa.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wapiganaji wa Al-Shabab, wanakadiriwa kuwa kati ya 7,000 na 9,000

Hili ni jambo tata ambalo limejadiliwa tangu mkutano wa kwanza wa London mwaka 2012.

Uhasama

Jimbo la Kusini Magharibi limekuwa na uhusiano wa kipekee na Ethiopia, nchi ambayo uhusiano wake na

Serikali kuu ya Mogadishu haujakuwa mwema. Hili linazua tatizo jingine: baadhi ya mataifa yamekuwa yakitia saini mikataba na serikali za majimbo.

Mfano, Umoja wa Milki za Kiarabu umekuwa ukitenga kambi ya kijeshi Somaliland, eneo ambalo serikali kuu ya Somalia huchukulia kuwa bado sehemu ya Somalia. UAE pia imetoa msaada wa zana za kivita kwa jimbo la Jubaland, kusini mwa Somalia.

Mjumbe maalum wa zamani wa Somalia nchini Marekani Abukar Arman, ameeleza Kongamano la Somalia kama "mkutano wa karamu", ambapo mataifa ya nje yamekutana kugawana Somalia kwa manufaa yao wenyewe.

Baadhi ya watu nchini Somalia wanatazama mkutano huo kama wa kupoteza muda tu.

"Wanasiasa na wanadiplomasia wameleweshwa na kongamano badala ya kuchukua hatua za kukabiliana an ukame," anasema Ahmed Mohamed, ambaye ni dereva wa bajaji Mogadishu.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Marekani ilianza kutahadhari baada ya helikopta mbili za Black Hawk kutunguliwa Somalia mwaka 1993

Lakini kuna mafunzo mengi ambayo wahusika wameyapata, na mtazamo kuhusu mzozo huo umebadilika kuliko ilivyokuwa miaka ya 1980.

Mwaka 1991, Marekani ilichukua hatua ya kutuma zaidi ya wanajeshi 30,000 kusaidia kukabiliana na ukame. Lakini waliondoka kwa aibu, baada ya helikopta mbili za Black Hawk kutunguliwa na wanamgambo wa kiukoo mwaka 1993.

Sasa, wengi wanazungumzia haja ya Wasomali wenyewe kumiliki shughuli hiyo, ingawa bado unaweza kuona "vivuli" vya mataifa ya nje yenye ushawishi.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii