Majaribio ya ndege mpya za Boeing yasitishwa

Boeing 737 MAX Haki miliki ya picha Getty Images

Shirika la ndege la Boeing limesitisha kwa muda safari za kufanyia majaribio ndege yake mpya ya 737 MAX kutokana na uwezekano wa kasoro kwenye injini za ndege hizo.

Hatua hiyo imechukuliwa siku chache kabla ya shirika hilo la ndege lenye makao yake Marekani kuwasilisha ndege za kwanza kwa mteja.

Lakini Boeing wamesema wataendelea na mpango wake wa kuanza kuwasilisha ndege hizo za MAX kwa wateja baadaye mwezi huu, na kwamba kampuni hiyo itaendelea kuunga ndege hizo kama kawaida.

American Airlines, Southwest, na shirika la Shandong Airlines la China ni miongoni mwa mashirika ambayo yameagiza ndege hizo.

Mapema mwaka huu, shirika la ndege la SpiceJet kutoka India liliwasilisha ombi la kununua ndege 205 mpya kutoka wka Boeing, ununuzi huo ukitarajiwa kuwa wa thamani ya $22bn (£18bn). Boeing wamesema ndege za kwanza za Max 737 zitawasilishwa kwa SpiceJet mwaka 2018.

Ndege za MAX zimeundwa kutotumia sana mafuta na zimeundwa kuchukua nafasi za ndege muundo wa 737 za awali, ambazo ziliuzwa kwa wingi sana na kampuni hiyo.

Boeing wanasema walifahamishwa wiki iliyopita kwamba huenda kuna kasoro kwenye injini za ndege hizo ambazo zilitengenezwa na kampuni ya kimataifa ya kuunda sehemu za injini ya CFM International.

CFM ni kampuni inayomilikiwa kwa pamoja na kampuni ya Marekani ya General Electric (GE) Safran ya Ufaransa na ndiyo iliyopewa kazi ya kuunda injini za ndege hizo za 737 Max.

Boeing wamesema hawakuwa wamepata taarifa zozote za hitilafu kwenye injini awali wakati was aa 2,000 za safari za majaribio.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Boeing 737 MAX 9 ilifanya safari yake ya kwanza Aprili

Ndege hiyo ya 737 MAX 8, inauzwa $110m lakini mashirika mengi ya ndege sana hupokea kipunguzo cha bei.

Muundo utakaofuata wa ndege hizo, 737 MAX 9, utakuwa na uwezo wa kubeba abiria wengi.

Kampuni ya Boeing ilisherehekea miaka 100 tangu kuanzishwa kwake mwaka jana.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii