Ujerumani kufunga biashara ya Korea Kaskazini

City Hostel Berlin Haki miliki ya picha EPA
Image caption Korea Kaskazini imeendesha biashara hiyo ya bweni kwa muda mrefu

Serikali ya Ujerumani inapanga kufunga biashara inayofaidi taifa la Korea Kaskazini katika jiji la Berlin.

Hatua hiyo, ya kufunga bweni kubwa ambalo linapatikana katika kipande kimocha cha ardhi na ubalozi wa Korea Kaskazini mjini Berlin, inaambatana na vikwazo vya Umoja wa Mataifa ambalo limewekewa taifa hilo.

Lengo la vikwazo hivyo ni kuzuia taifa hilo la kikomunisti kustawisha silaha zake za nyuklia.

Bweni hilo kwa jina City Hostel Berlin huendeshwa na kampuni ya biashara za hoteli ya Uturuki ambayo hulipa zaidi ya €38,000 (£32,000; $41,000) kama kodi kwa Korea Kaskazini.

Ubalozi wa Korea Kaskazini mjini Berlin pia hujipatia mapato kwa kukodisha ukumbi ulio katika eneo palipojengwa bweni hilo.

Korea Kaskazini imetekeleza majaribio kadha ya silaha za nyuklia na pia majaribio ya makombora ya masafa marefu.

Hilo limeibua wasiwasi kwamba huenda karibuni ikawa na makombora ya nyuklia yanayoweza kufikia Japan au Marekani.

City Hostel Berlin ilijengwa zamani katika Ujerumani Mashariki ambayo ilikuwa ya Kikomunisti kabla ya kuungana tena kwa taifa hilo na Ujerumani Magharibi na kuwa Ujerumani ya sasa.

Bweni hilo lilitumiwa kama makazi ya wafanyakazi wa ubalozi.

Ni maarufu sana kwa watu wanaosafiri Berlin kutokana na gharama yake nafuu.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Bweni hilo huwa nafuu kwa wageni

Inakadiriwa kwamba mgeni anaweza kukaa katika bweni lenye vitanda vinane kwa kulipa €9.50 kila siku.

Azimio 2321 la Umoja wa Mataifa ambalo liliidhinishwakwa kauli moja Novemba mwaka jana lilikaza vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini baada ya taifa hilo kufanya jaribio la silaha za nyuklia tarehe 9 Septemba.

Azimio hilo huyataka 2mataifa yote wanachama kuizuia DPRK [Korea Kaskazini] kutumia nyumba ama ardhi inayomiliki au kukodi katika mataifa husika kwa matumizi mengine ila shughuli za kibalozi".

Markus Ederer, katibu katika Wizara ya Mambo ya Nje wa Ujerumani, amesema "ni sharti tuongeze shinikizo ili kuhakikisha Korea Kaskazini inarejea kwenye meza ya mazungumzo."

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Bweni hilo linapatikana katika kipande kimoja cha ardhi na ubalozi wa Korea Kaskazini

Vikwazo hivyo vya Umoja wa mataifa vinafaa kutekelezwa kikamilifu, alisema, "kwa hivyo ni muhimu sana tuzime shughuli ambazo zinaweza kutumiwa kupata pesa za kufadhili mpango wa nyuklia (wa Korea Kaskazini)".

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii