Trump amuonya mkuu wa FBI aliyefutwa James Comey

Donald Trump Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Trump amesisitiza kwamba aliambiwa na Comey kwamba hachunguzwi na FBI

Rais wa Marekani Donald Trump amemtahadharisha mkuu wa shirika la uchunguzi wa jinai FBI aliyefutwa kazi James Comey dhidi ya kufichua habari kwa vyombo vya habari.

Bw Trump ameandika kwenye Twitter kwamba Bw Comey heri "atumai kwamba hakuna kanda zozote kuhusu mazungumzo yetu".

Bw Comey, ambaye amekuwa akiongoza uchunguzi kuhusu uwezekano wa ushirikiano kati ya maafisa wa kampeni wa Bw Trump na serikali ya Urusi alifutwa kazi Jumanne.

Bw Trump baadaye alisema aliambiwa na Bw Comey kwamba yeye mwenyewe hakuwa anachunguzwa.

Bw Trump amesema kwamba alikuwa amehakikishiwa mara mbili na Bw Comey, mara moja wakati wa dhifa ya jioni na mara ya pili kwa njia ya simu kwamba hakuwa anchunguzwa.

Rais huyo amesema: "Nilisema: 'Ikiwezekana, unaweza kunifahamisha: je ninachunguzwa?' Alinijbu: 'Hauchunguzwi.'"

Bw Trump alisema wiki hii kwamba alichukua hatua ya kumfuta Bw Comey mwenyewe.

Wakati wa kumfuta, alimweleza kama mtu asiye wa kuaminika na mtu mwenye kujitakia sifa.

Hilo lilionekana kwenda kinyume na tamko la maafisa wa uatawala wake kwamba Bw Comey alifutwa kutokana na mapendekezo ya Mwanasheria Mkuu jeff Sessions na naibu wake Rod Rosenstein.

Mstari wa kwanza wa barua ya Bw Trump ya kumfuta Bw Comey inarejea barua iliyoandikwa na Bw Rosenstein na inasema: "Nimekubali mapendekezo yao."

Katika ujumbe mwingine kwenye Twitter Ijumaa, Bw Trump alizungumzia tofauti hizo, na kusema: "Mimi ni Rais mwenye shughuli nyingi na shughuli nyingi zinafanyika, haiwezekani kwa watu wangu kusimama jukwaani na kusema jambo kunihusu kwa ufasaha kabisa!"

Aliongeza: "pengine, njia bora zaidi kwangu kufanya inaweza kuwa kwangu kufuta "vikao vya kuwapasha wanahabari" na badala yake niwe nikitoa ujumbe ulioandikwa kwa ajili ya kufanya mambo yote yawe sahihi???"

Bw Trump alipuuzilia mbali uchunguzi unaofanywa na FBI na akasema wafuasi wa Democratic wanatumia "taarifa za uongo" kutuhumu maafisa wake wa kampeni kwamba walikuwa na uhusiano na maafisa wa Urusi.

Aliandika katika ujumbe mwingine: "James Clapper mwenyewe (mkuu wa zamani wa Idara ya Taifa ya Ujasusi), na karibu kila mtu aliyekuwa na ufahamu kuhusu kisa hiki cha kuwinda maafisa wangu, aliposema hakukuwa na uhusiano wowote, ni lini haya yataisha?"

Haki miliki ya picha Google
Image caption Mkurugenzi wa zamani wa FBI James Comey

Lakini mrithi wa Comey, kaimu mkuu wa FBI Andrew McCabe, alisema Alhamisi kwamba uchunguzi huo unasalia kuwa "uchunguzi muhimu".

Akitoa ushahidi mbele ya kamati ya Seneti kuhusu ujasusi, aidha, alitilia shaka madai ya ikulu ya White House kwamba Bw Comey alikuwa amepoteza imani machoni pa wafanyakazi wake.

"Ninaweza kuwaambia kwa imani kwamba wengi wa wafafanyakazi wana uhusiano wa ndani na uliokolea na Mkurugenzi Comey," Bw McCabe alisema.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii