Msichana wa Chibok asema hawezi kurudi nyumbani kwa sababu wazazi wake hawatakubali kubadilisha dini

Uislamu wamfanya msichana wa Chibok kutorudi nyumbani
Maelezo ya picha,

Uislamu wamfanya msichana wa Chibok kutorudi nyumbani

Kundi la wapiganaji wa Boko Haram limetoa kanda ya video inayodai kuonyesha wasichana wanne waliokataa kurudi nyumbani ili kujiunga na familia zao.

Wiki moja iliopita wasichana 82 kati yao waliachiliwa huru baada ya miaka miwili wakiwa chini ya watekaji wao.

Waliachiliwa baada ya serikali pia kuwaachilia makamanda watano wa Boko Haram .

Kuna takriban wasichana 100 wa Chibok waliosalia na wapiganaji hao huku serikali ya Nigeria ikisema kuwa mazungumzo ya kuwaachilia huru yanaendelea.

Mmoja ya wasichana hao alionekana akibeba bunduki huku mwengine akisema kuwa hangependelea kurudi nyumbani kwa sababu familia yake haiwezi kubadilika na kuwa Waislamu.

Wasichana 82 walioachiliwa wikendi iliopita wanasubiri kuunganishwa na familia zao lakini wataendelea kuangaliwa na serikali.

Msemaji wa afisi ya rais anasema kuwa msichana mwengine alitarajiwa kuachiliwa lakini akakataa.

Inadaiwa kuwa wasichana wengine waliolewa na watekaji wao na wamepata watoto.