Korea Kaskazini: Kombora jipya lina uwezo wa kubeba nyuklia

Gwaride la kijeshi lililofanywa na Korea Kaskazini hivi karibuni Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Gwaride la kijeshi lililofanywa na Korea Kaskazini hivi karibuni

Korea Kaskazini imedai kwamba kombora la masafara marefu ililolifanyia majaribio siku ya Jumapili ni kombora jipya linaloweza kubeba kichwa cha nyuklia .

Kombora hilo lililorushwa lilienda anagani urefu wa kilomita 2,000 na kusafiri kilomita 700 kabla ya kuanguka katika bahari Magharibi mwa Japan.

Korea Kaskazini ilisema siku ya Jumatatu ni jaribio la uwezo wa kombora jipya.

Jeshi la Korea Kusini limesema kuwa haliweza kuthibitisha madai hayo ya Korea Kaskazini.

Lakini limesema kuwa kombora hilo lilionekana kuweza kuruka angani, hatua ambayo ni muhimu katika utengenezaji wa makombora ya masafa marefu kulingana na kituo cha habari cha Yonhap.

Majaribio ya mara kwa mara ya makobora ya masafa marefu yanayofanywa na taifa hilo yanakiuka vikwazo vya Umoja wa Mataifa na yamesababisha wasiwasi miongoni mwa jamii ya kimataifa pamoja na Marekani.

Marekani na Japan zimetaka kufanyika kwa mkutano wa dharura katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa siku ya Jumanne.

Shirika la habari la Korea Kaskazini KCNA limesema Jumatatu kwamba jaribio la kombora jipya la masafa marefu la Hwasong 12 lilifanyika kama ilivyopangwa.

Limesema kuwa jaribio hilo lililenga kuonyesha kwamba kombora hilo jipya lina uwezo wa kubeba kichwa cha Nyuklia.

Mada zinazohusiana