Uchaguzi wa Kenya: Maswali muhimu na majibu

Mpiga kura nchini Kenya Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mpiga kura nchini Kenya

Kabla ya uchaguzi utakaofanyika nchini kenya mwezi Agosti, kuna baadhi ya maswali ambayo wengi wa wasomaji wamekuwa wakiuliza.

Tutakuwa tukiongezea maswali mapya katika ukurasa huu, kadiri siku zinavyosonga.

Je kabila la mtu lina umuhimu katika uchaguzi?

Viongozi wa kisiasa nchini Kenya wamekuwa wakitegemea sana kuungwa mkono na watu wa kabila lao na hakutakuwa na tofauti wakati huu.

Kwa hivyo si ajabu kwamba baadhi ya wachambuzi wa kisiasa wamekuwa wakichambua sajili za wapiga kura katika ngome za wagombea na kuitumia kama kiashiria cha wale ambao wana nafasi nzuri ya ushindi.

Asilimia 70 ya watu nchini Kenya wanatoka katika kabila tano kubwa. Ili kunyakua kiti cha urais, mgombeaji anahitaji kuwa na ushirikiano wa kikabila ili kupata idadi kubwa ya kura hiyo.

Ukabila pia una nafasi kubwa katika uchaguzi wa wabunge, maseneta, magavana na kadhalika.

Hata hivyo Rais Uhuru kenyatta aliiambia Financial Times kuwa anatarajia uchaguzi huu kufanyika kwa misingi ya kiuchumi, hasa kuongezeka kwa gharama ya chakula.

Upinzani umeishutumu serikali kwa kushindwa kutatarajia uhaba wa chakula kutokana na ukame unaoendelea.

Vilevile, imeishutumu serikali kwa kusababisha uhaba bandia wa chakula ili kuruhusu wafanyabiashara walio na ushirika na serikali, kutumia kipindi cha dharura kuagiza mahindi, ambacho ni chakula kikuu, bila kulipa ushuru.

Serikali imekanusha madai haya na sasa imetoa ruzuku kwa unga wa mahindi.

Inaweza kuwa ni kweli wapiga kura watashawishiwa na masuala mengine mbali na ukabila.

Utafiti mmoja wa mwezi Aprili ulionyesha kuwa asilimia 28 ya wapiga kura walikuwa hawajaamua ni nani watampigia kura.

Ni mgombea yupi atawaondoa wanajeshi wa Kenya nchini Somalia?

Rais Kenyatta amesema kuwa wanajeshi wa Kenya watabaki Somalia hadi pale amani na utulivu utarejea nchini humo tena.

Kenya ina wanajeshi 3,600 wanaohudumu chini ya Amisom nchini Somalia. Walienda huko mwaka wa 2011 baada ya shambulizi kadhaa za al-Shabab.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Wanajeshi wa Kenya wako Somalia chini ya Amisom

Lakini muungano wa upinzani, Nasa, umesema utawaondoa askari wa Kenya nchini Somalia, na kusema kwamba wanahitajika zaidi, nyumbani.

Kuanza 2011, wapiganaji wa al-Shabab wametekeleza shambulizi kadhaa nchini Kenya, ikiwemo ile ya Westgate mwaka wa 2013 na ile ya chuo kikuu cha Garissa ambapo wanafunzi 148 waliuawa.

Januari mwaka jana, askari 150 wa KDF waliripotiwa kuuawa baada ya al-Shabab kuivania kambi ya kijeshi. Wengine walikamatwa na wameonekana katika vide za propaganda za wapiganaji hao.

Serikali ya Kenya bado haijatoa idadi rasmi ya askari waliouawa au kutekwa nyara katika shambulio hilo.

Je, tume ya uchaguzi itaweza kuendesha uchaguzi wa kuaminika?

Timu mpya ya maafisa wa uchaguzi iliingia ofisini Januari baada ya timu ya awali kushutumiwa kwa kutosimamia uchaguzi wa 2013 vizuri.

Hukumu juu ya uaminifu wa uchaguzi utapitishwa baada ya Agosti 8.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Chebukati anasema kuwa timu yake imejitayarisha vyema kusimamia uchaguzi.

Tume ya uchaguzi inasema kuwa inaangalia baadhi ya changamoto zilizokuwepo katika uchaguzi wa 2013, kama vile ukosefu wa mafunzo kwa wafanyakazi wake juu ya matumizi ya teknolojia ya kupiga kura na vituo kuchelewa kupata vifaa vya uchaguzi.

Tume hiyo ina mfumo maalumu wa usimamizi wa uchaguzi (KIEMS) ambao kwa sasa unatumika kuthibitisha uandikishaji wa wapiga kura na utatumika siku ya uchaguzi kuthibitisha wale wanaofaa wapiga kura, matokeo ya uchaguzi na hata usambazaji wa matokeo ya kura kwa kituo cha kitaifa cha kuhesabu kura.

Mwenyekiti wa tume hiyo, Wafula Chebukati aliwaeleza wanahabari mwezi Mei kuwa wafanyikazi wake tayari wanajifunza kutumia mfumo huo maalum na hawatangoja hadi dakika za mwisho kuwapa nafasi hiyo, kama ilivyofanyika.

Mwezi Februari, asilimia 65 wallioshiriki utafiti walisema wana imani na tume hii.

Mitandao ya kijamii inatumiwa vipi katika kampeni?

Mitandao ya kijamii ina nafasi kubwa sana katika uchaguzi huu kuliko zamani.

Wakenya wengi wanatumia mtandao wa Twitter na wanajulikana kama KOT (Kenyans on Twitter). Wana msukumo mkubwa katika kampeni na wanaitumia mitandao kuuza sera za wale wanaowaunga mkono.

Vyama vya kisiasa pia vimeajiriwa wahamasishaji ambao wana wafuasi wengi katika mitandao ya jamii kushinikiza ujumbe wao.

Pia kuna wale wameajiriwa kuandika na kunena mambo mazuri mazuri, ya kuipa chama nafasi nzuri katika mitandao na kuweka kampeni kali dhidi ya wale wanaosema mabaya kuhusu chama.

Wengine wana mbinu wanazotumia kuonekana kwamba wana wafuasi wengi sana kwenye twitter.

Vyombo vikuu vya habari pia vinatumia Facebook, YouTube na Twitter kutangaza mikutano ya kisiasa na programu maalum.

Wagombea wakuu wa urais hasa wamejitokeza sana. Rais Kenyatta amekuwa akitoa ujumbe wa umoja na maendeleo:

Haki miliki ya picha TWITTER/RAIS WA KENYA

Huku kiongozi wa upinzani Raila Odinga akisema kwamba anaungwa mkono na wapiga kura milioni 10. Kampeni Odinga inasema kwa kimsingi kuwa wao wana nafasi nzuri zaidi ya kushinda uchaguzi kwa sababu idadi ya wapiga kura halali ni milioni 19.

Haki miliki ya picha TWITTER/RAILA ODINGA

Waziri wa usalama wa ndani amekuwa akisema upinzani unaleta wasiwasi kwa wananchi kwa kusema haya, lakini chama cha Kenyatta pia kimekuwa kikisukuma ujumbe kwamba kitashinda uchaguzi kwa kupata asilimia 70 ya kura.

Kuna maelfu ya wagombeaji lakini sio wote wanaopata nafasi katika vyombo vikuu vya habari na hivyo wengi, hasa wagombea wa kujitegemea, wanatumia majukwaa ya kijamii kama Facebook Live

Wanasiasa wanachangisha vipi fedha za kutumia katika kampeni?

Kenya haina sheria zinazosimamia jinsi wanasiasa wanavyochangisha fedha za kutumia wakati wa kampeni.

Jaribio la tume ya uchaguzi kuwasilisha bungeni mswada wa kudhibiti fedha za kampeni lilizimwa na wabunge.

Tume hiyo ilikuwa imetoa mapendekezo yafuatayo kwa viti tofauti.

  • Rais: $50m
  • Magavana: $4m
  • Wabunge na Maseneta: $290,000
  • Wawakilishi wa Wadi: $97,000

Kutokuwa na sheria hii kuna maana kuwa wagombeaji wana uhuru ya kutumia pesa vile wanavyotaka.

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation, "Mara nyingi fedha hizo hutumika kufanya mipango na kugharimia matangazo lakini wagombea wengi na vyama pia huzitumia kuwahonga wapiga kura".

Gazeti hilo liliripoti kuwa katika uchaguzi wa 2013, muungano wa upinzani wakati huo Cord, ulitumia zaidi ya $50m (£40m) huku mrengo unaotawala wa Jubilee ukitumia zaidi ya $100m kuendesha kampeni za urais.

Wanasiasa huchangisha pesa kutoka wafanyibiashara na wengine hufanya harambee. Vyama vya upinzani hata hivyo vimekuwa vikikishutumu chama tawala kwa kutumia rasilimali za serikali katika kampeni.

Je, kutakuwepo na ghasia baada ya uchaguzi?

Ken Opalo, kutoka chuo kikuu cha Georgetown nchini Marekani, anasema ijapokuwa kuna dalili za uwezekano wa kutokea kwa fujo, hali haitakuwa mbaya kama iliyoshuhudiwa miaka 10 iliyopita, wakati watu zaidi ya 1,000 walifariki dunia na 600,000 kufurushwa makwao.

"Sina wasiwasi sana kuhusu uchaguzi mkuu katika ngazi ya taifa. Wasiwasi sana ni katika kaunti," aliongeza.

"Ghasia kwa uhakika zitakuwepo. Lakini, sana zitakuwa ni za kuangazia ushindani mkali utakaokuwepo wakati huo, badala ya kusambaratika kabisa kwa mifumo ya dola na kutanda kwa ghasia."

Bw Nic Cheeseman, Profesa wa masuala ya demokrasia katika Chuo kikuu cha Birmingham Uingereza na ambaye pia ni mchanganuzi wa siasa za Kenya, ana msimamo sawa na huo.

Anasema kuwa: "Mtafaruku ulioshuhudiwa wakati wa kufanyika kwa uchaguzi wa mchujo katika vyama vya siasa ni jambo la kuzua wasiwasi, lakini kwamba huenda kusiwepo na ghasia sana wakati wa uchaguzi mkuu."

Uchumi wa Kenya upo katika hali gani?

Kenya imedumisha ukuaji thabiti wa uchumi kwa miaka tano iliyopita, ambapo uchumi umekua kwa asilimia 5% kila mwaka.

Hata hivyo, kupanda kwa bei ya bidhaa muhimu za kawaida kama maziwa, mkate na unga kumesukuma juu mfumuko wa bei kwa asilimia 12%, na familia nyingi nchini Kenya zimekuwa zikitatizika kujikimu .

Wakenya wamekuwa wakitumia kitambulisha mada #CostOfLivingKe (Gharama ya kuishi Kenya) kujadili kupanda bei kwa bidhaa za kawaida na jinsi wanavyobadilisha mitindo yao ya kuishi.

"Kila mwaka wa uchaguzi, uchumi pia huenda chini na hali ndiyo iyo hiyo mwaka huu huku wawekezaji wakingojea kuona jinsi uchaguzi utakavyoenda," Kwame Owino, Mkurugenzi Mkuu katika taasisi ya masuala ya uchumi aliiambia BBC.

"Baadhi ya kampuni zinapunguza idadi ya wafanyakazi, sekta isiyo rasmi ikiwa mwajiri mkubwa," aliongezea.

Mazuri:

Kenya ilipata uwekezaji wa jumla ya $1bn, baada ya kufanya mageuzi mbalimbali kama vile kama kupunguza kwa gharama ya kufanyia biashara na urasimu, uwekezaji katika miundombinu na kupunguzwa kwa gharama ya viza jambo ambalo limeimarisha utalii.

Mabaya:

Hata hivyo uchumi umekumbwa na kukita mizizi kwa utoaji wa rushwa, uhasama wa kisiasa na hatua ya serikali kudhibiti viwango vya riba - njia iliyokuwa ipunguze gharama ya mikopo lakini haijafanikiwa.

Shirika la maendeleo la umoja wa mataifa (UNDP) linasema kuwa Kenya ina kiwango cha ukosefu wa ajira cha juu zaidi katika kanda hii, huku watu wanne kati ya kumi wakiwa hawana kazi.

Bw Owino anasema kuwa wapigaji kura ambao hawajaridhishwa na serikali wanaweza kuunga mkono wale wanaodhania watajali mahitaji yao ya kiuchumi.

Ufisadi ni mbaya kiasi gani?

Katika ripoti yake ya 2016, shirika la Transparency International liliweka Kenya katika nafasi ya 145 kati ya nchi 176 kwa kukithiri kwa rushwa.

Ililaumu nafasi hiyo chini ya Kenya kwa uzembe na kukosa ufanisi wa mashirika ya kupambana na ufisadi, ikisema kukosa kuadhibu waliopatikana wakishiriki katika ulaji rushwa kumekuwa kikwazo kikubwa.

Mwanaharakati wa kupambana na ufisadi John Githongo ameitaja serikali ya rais Uhuru Kenyatta kama "iliyo na ufisadi mkubwa katika historia ya Kenya".

Rais Kenyatta hata hivyo amesema kuwa juhudi zake za kupambana na ufisadi zinadhoofishwa na mahakama, ambayo inashughulikia kesi hizo kwa mwendo wa kinyonga, na kulitaja shirika na kupambana na ufisadi kuwa vivu mno.

Bw Githongo alitaja ripoti kadhaa za kashfa inayoshirikisha madai ya kupandishwa kwa bei ya miradi na malipo kwa kampuni hewa.

Mwakani 2015, Kenyatta aliwasimamisha kazi na hatimaye kuwatoa ofisini mawaziri watano na maafisa wa juu serikalini kwa madai ya ufisadi.

Waziri mmoja alijiuzulu baada ya shinikizo kutoka kwa umma.

Wanachama wa upinzani pia wametajwa katika kashfa kadhaa, lakini wengine wameilaumu serikali kwa kuwasingizia.

Mashirika ya kikatiba yaliyobuniwa kupambana na ufisadi yameshutumiwa kuwa hawana msimamo wao binafsi.

Mdadisi wa masuala ya siasa nchini Kenya Barrack Muluka anawalaumu Wakenya wa kawaida kwa tatizo katika kukabiliana na ufisadi, akisema kuwa wamefumbwa macho na ukabila: "Serikali yaweza kuiba itakavyo na Wakenya watafurahia ikiwa tu ni "wezi wetu."

Aligusia uchaguzi wa mchujo mwezi Aprili ambapo wagombeaji waliokuwa na utata kuhusu uadilifu wao na wale waliodaiwa kushiriki katika ufisadi bado walishinda uchaguzi wa mchujo.

Bw Githongo anaitaja hatua hiyo kuwa sawa na " kuhalalisha upuuzi"

Anasema kuwa wizi umekuwa jambo la kawaida: "Wale tuliowaita wezi sasa ni watu waliopambana na kufanikiwa maishani."

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii