Israel: Uhusiano wetu na Marekani haujaharibiwa na Urusi

Trump anatarajiwa kutembelea Israel wiki ijayo
Image caption Trump anatarajiwa kutembelea Israel wiki ijayo

Israel imesema uhusiano wake na Marekani haujaharibiwa na tuhuma kwamba Rais Trump ameipa Urusi taarifa za siri alizopewa na Israel.

Balozi wa Israel nchini Marekani, Ron Dermer, amesisitiza kwamba nchi yake bado ina imani na Marekani katika uhusiano wao wa kupeana taarifa za ki-intelijensia.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani amekataa kuzungumzia tuhuma hizo.

Mwanzoni, Rais Trump ametetea kile alichokiita haki yake ya msingi kupeana taarifa zinazohusu masuala ya ugaidi na usalama wa angani.

Wiki ijayo, Rais Trump atatembelea Israel.

Wakati huo huo, mwanasiasa wa ngazi ya juu wa chama cha Democrat katika bunge la Senate Chuck Schumer ametaka ikulu ya Marekani kutoa taarifa za maandishi za mkutano huo.

Rais Donald Trump kwa mara nyingine amegubikwa na utata huku utawala wake ukikana taarifa kwamba amelitaka shirika la ujasusi la FBI kusitisha uchunguzi wa aliyekuwa mshauri wake wa masuala ya usalama wa taifa, Michael Flynn.

Image caption James Comey alifutwa kazi na Trump wiki iliyopita

Ikulu ya Marekani imesema ripoti iliyopo kwenye gazeti la New York Times na vyombo vingine vya Marekani haikuwa ya kweli au haikuonyesha uhalisia wa mazungumzo ya mwezi February baina ya Rais na aliyekuwa wakati huo mkurugenzi wa FBI, James Comey.

Tuhuma hizo zinahusisa maagizo yanayodaiwa kuandikwa na bwana Comey baada ya kukutana na Rais Trump.

Trump alimfuta kazi Comey wiki iliyopita.