Wafungwa wauawa wakijaribu kutoroka jela DRC

Maafisa wa usalama waendesha Operesheni mji Kinshasa
Image caption Baadhi ya magereza nchini DRC yamekjuwa yakishuhudia kutoka kwa wafungwa kutokana na msongamano ulioko

Idadi ya wafungwa wasiojulikana wameuawa kwa kupigwa risasi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mapema leo baada ya jaribio la kuhepa kutoka gereza kubwa lililoko mjini Kinshasa.

Waziri wa sheria nchini humo, Alexis Thambwe Mwamba amesema baadhi ya wafungwa wapatao 100 wamekamatwa huku wengine hamsini na watano wakiendelea kusakwa.

Miongoni mwa wanaodaiwa kufanikiwa kutoroka ni mfungwa mmoja aliyekuwa akitumikia kifungo cha maisha gerezani kwa mauaji ya rais wa zamani wa DRC, Laurent Kabila.

Maafisa wa usalama wameanzisha oparesheni kali mjini Kinshasa ili kuwakamata wafungwa hao.

Aidha, baadhi ya wafungwa wameuawa kwa kupigwa risasi wakijaribu kukimbia .

Mwandishi wa BBC mjini Kinshasa anasema amewaona maafisa wa shirika la Msalaba Mwekundu, wakikusanya miili yao.

Miili ya waliofariki imepelekwa katika vyumba vya kuhifadhia maiti mjini Kinshasa.

Mapigano makali DRC

Mahakama DRC yaidhinisha kuahirisha uchaguzi

Hii sio mara ya kwanza kwa wafungwa kutoroka kutoka magereza nchini DRC kwani Januari mwaka uliopita, kisa kama hicho kilishuhudiwa mashariki mwa taifa hilo ambapo wafungwa hamsini walitoroka.

Miongoni mwa waliofanikiwa kutoroka ni wafungwa wa kesi za mauaji na ubakaji.

Mamlaka za magereza zimelaumiwa kwa visa hivyo kwa ulegevu huku magereza mengi yakiwa na msongamano.

Mashirika ya kutetea haki za kibanadam yanalaumu idara ya mahakama kwa kutokamilisha kesi haraka.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii