Msanii Juliani atoa wimbo kuhusu mauaji ya kiholela Kenya

Msanii Juliani Haki miliki ya picha Facebook
Image caption Mwanamziki huyo amekuwa akizungumzia masuala ya kisheria katika nyimbo zake

Msanii maarufu nchini Kenya, Juliani, ambaye jina lake halisi ni Julius Owino, ametoa wimbo unoazungumzia mauaji ya kiholela dhidi ya raia nchini humo.

Juliani, anayefahamika kwa tungo zinazoangazia masuala ya maadili na haki za kibanadamu, ameachia wimbo, 'machozi ya jana' alioutunga kuhusu mauaji na ukiukaji wa haki za kibanadamu.

Msanii huyo amegusia pakubwa mauaji ya wakili Willy Kimani kutoka shirika la International Justice, aliyeuawa mwaka jana akiwa na mteja wake, Josephat Mwenda na dereva wa teksi, Joseph Muiruri.

Watatu hao walitoweka wakiondoka mahakamani mashariki mwa Kenya kabla ya miili yao kupatikana wameuawa mnamo mwezi Juni 2016.

Maafisa wanne wa polisi, wakiwemo, Fredrick ole Leliman, Leonard Mwangi Maina, Sylvia Wanjiku Wanjohi na Stephen Morogo wanazuiliwa huku wakikabiliwa na mashtaka ya kutekeleza mauaji hayo.

Mbali na hayo, wimbo huo uliojaa huzuni, unaangazia changamoto za familia za waathiriwa wa mauaji hayo ya kiholela zikiwemo kucheleweshwa kwa kesi hizo.

Mashirika mbalimbali ya kutetea haki za kibinadamu nchini Kenya yamekuwa yakiishinikiza serikali kukomesha mauaji ya kiholela huku maafisa wa usalama wakidaiwa kutekeleza baadhi ya mauaji hayo.

Mada zinazohusiana