Trump aipa Tanzania $526m kukabiliana na ukimwi

Rais wa Marekani Donald Trump Haki miliki ya picha AFP
Image caption Marekani inaendesha miradi mbalimbali ya afya kupitia PEPFAR katika mataifa mengi Afrika

Serikali ya Marekani kupitia ofisi ya rais Donald Trump imetangaza kupatia Tanzania ufadhili wa kukabilana na virisu vya ukimwi.

Marekani, ambayo siku chache zilizopita ilitangaza kusimamisha ufadhili wake kwa wizara ya afya nchini Kenya, imeipa Tanzania kitita cha dola milioni 526.

Kitita hicho kutoka mfuko wa PEPFAR, kitatumika kufanikisha mpango wa kutoa huduma kwa zaidi ya watu milioni 1.2 wanaoishi na virusi hivyo.

Akizungumza baada ya tangazo hilo, mwakilishi wa ubalozi wa Marekani nchini Tanzania, Virginia Blaser amesema kuwa wanalenga kufanikisha kizazi kilicho huru kutoka virusi nchini Tanzania.

''Kwa niaba ya raia wa Marekani, tunafurahia ushirikiano wetu na Tanzania na tunajitahidi kuhakikisha hakuna anyeachwa nje," Alisema.

Miongoni mwa huduma hizo ni matibabu, ukaguzi, na kuzuia maambukizi mapya ya virusi hivyo kuanzia sasa hadi Septemba mwaka ujao.

Halikadhalika, serikali ya Marekani itashirikiana na serikali ya Tanzania kutekeleza huduma za kuwapima raia milioni 8.6 ili kuwawezesha kujua hali yao ya virusi.

Pesa hizo pia zitatumika kuimarisha maisha ya wajane na mayatima wa viurusi hivyo, kuzuia dhulma za kijinsia, pamoja na kuwafikia zaidi ya watu laki tatu walioambukizwa.

Mashirika mbalimbali yanayoendesha miradi mbalimbali ya afya nchini Tanzania, kama vile (TACAIDS), na wakfu wa rais mstaafu, Benjamin Mkapa (Benjamin Mkapa HIV/AIDS Foundation (BMAF)) yanatarajiwa kushiriki kufanikisha mpango huo.

Mapema mwezi huu, Marekani ilikatiza ufadhili wake wa miradi kama hivyo nchini Kenya pamoja na kuyazuia mashirika dhidi ya kufanikisha miradi yoyote na wizara ya afya ya taifa hilo kutokana na usimamizi mbaya wa fedha.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii