Mtu achomwa Venezuela huku idadi ya vifo ikiongezeka

Onyo: Baadhi ya picha katika taarifa hii huenda zikaudhi

Polisi wakabiliana na waandamanaji Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Watu kadhaa wameuawa na mamia kujeruhiwa kufuatia wiki kadhaa ya maandamano ya kupinga serikali

Rais wa venezuela Nicolas maduro amesema kuwa waandamanaji wanaounga mkono upinzani ndio walimwasha moto raia mmoja anayeunga mkono serikali huko Caracas, katika siku ya 50 ya maandamano.

Orlando José Figuera aliungua asilimia 80 ya mwili wake . Maafisa wanasema kuwa alidungwa kisu pia katika maandamano ya jumamosi.

Mashahidi wanasema kuwa umati ulidai kuwa alikuwa mwizi.

Siku hiyo hiyo, mwanaharakati wa upinzani alipigwa risasi, na kusababisha idadi ya watu ambao wameuawa katika maandamano ya hivi karibuni kufika 48.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Orlando José Figuera aliungua asilimia 80 ya mwili wake na kudungwa kisu katika maandamano

Ofisi ya mwanasheria mkuu ilisema watu waliokuwa na bunduki walianza kuwafyetulia risasi waandamanaji katika mji wa Valera.

Edy Alejandro Teran Aguilar alifariki kutokana na jeraha la risasi kifuani, huku wengine wawili wakijeruhiwa.

Waandamanaji wanaomtaka Rais Maduro kujiondoa mamlakani na uchaguzi kuandaliwa walijaa mitaani na barabarani nchini kote siku ya Jumamosi, kuadhimisha siku 50 za maandamano ambazo inazidi kuleta vurugu nchini.

"Mtu alichomwa na kupigwa vibaya kisha akadungwa kisu...karibu wamuue kwa sababu tu alitamka kuwa yeye ni 'Chavista'," Rais Maduro alisema, akiashiria chama tawala cha Socialist kilichoanzishwa na mtangulizi wake Hugo Chavez.

Inadhaniwa watu 46 walijeruhiwa katika maandamano hayo ya Caracas mashariki ambapo Figuera, mwenye umri wa miaka 21 aliumizwa.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Orlando José Figuera alidaiwa kuwa mwizi.

Maandamano dhidi ya rais Maduro na serikali yake yamekuwa yakiendelea Venezuela kwa wiki saba, sasa.

Watu saba kati ya 10 wanasemekana kumpinga Maduro, kwa mujibu wa tafiti binafsi.

Licha ya kuwa na akiba kubwa zaidi ya mafuta duniani, Venezuela inakabiliwa na uhaba wa vitu vingi vya msingi, ikiwa ni pamoja na chakula na madawa.

Uchumi wake umeanguka, huku mfumuko wa bei ukitarajiwa kuwa juu ya asilimia 700%mwaka huu.Uhalifu pi aumeongezeka.

Upinzani unataka uchaguzi wa mapema ufanywe na kuachiliwa kwa wanasiasa wa upinzani waliokamatwa na kuwekwa jela katika miaka ya karibuni,. Inasema serikali ya ujamaa ya Maduro na mtangulizi wake, marehemu Hugo Chavez, imeharibu uchumi.

Mada zinazohusiana