Mlipuko waua 19 Manchester

Polisi wakiendelea na ulinzi eneo la tukio Haki miliki ya picha Peter Byrne
Image caption Polisi wakiendelea na ulinzi eneo la tukio

Watu 19 wamefariki dunia na wengine 50 kujeruhiwa baada ya kutokea mlipuko wakati wa tamasha la muziki katika uwanja wa Manchester, Uingereza.

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May ametaja tukio hili kama kitendo cha ugaidi.

Ikiwa itathibitishwa kuwa ni shambulio la kigaidi, litakua mbaya zaidi kuwahi kukumba Uingereza tangu Julai mwaka 2005 wakati zaidi ya watu 50 walikufa kwenye mfululizo wa milipuko mjini London.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Ulinzi umeimarishwa

Mashahidi nao walioshuhudia tukio hilo wanasema mlipuko mkubwa uliosababisha jengo zima kutingishika, ulitokea mara tu baada ya mwimbaji wa Kimarekani Ariana Grande kumaliza onyesho lake.

'' Niliona wazazi na watoto wakikimbia nje huku damu zikiwa zimewatapakaa mwili mzima. Nimemchukua mwanamke huyu, ambaye anasema alikuwa akiwatafuta wajukuu zake. Hajawapata. Alimuokota tu binti aliyekuwa amedondoka chini akiwa ametapakaa damu na wazazi wake walikuwa wamelala karibu yake. Ni ajabu isiyo ya kawaida. Nimesaidia watu waliokuwa wakitopa nje huku wakiwa wameloa damu. Ulikuwa ni mshtuko...'' alisema Andy Royal.