Shambulizi la Manchester: Tunafahamu nini?

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Manusura wakitoroka eneo la shambulizi

Watu 22 wameuwawa na 59 kujeruhiwa kwenye mlipuko wakati wa tamasha la mwanamuziki Mmarekani Arana Grande kwenye ukumbi wa Manchester nchini Uingereza

Haya ndiyo yale tunayoyafahamu

Ni kipi kilitokea?

Mlipukoa ulitokea kwenye ukumbi wa Manchester siku ya Jumatatu usiku wakati watu walianza kuondoka kwenye tamasha.

Walioshuhudia walisema kuwa waliona vipande vya chuma kwenye sakafu na harufu ya milipuko baada ya bomu hilo la kutengezewa nyumbani kulipuka.

Pia walizungumzia hofu na hali ya kuchanganyikiwa iliyowakumba wale waliohudhuria tamasha.

Polisi waliitwa na barabara zinazozunguka ukumbi huo na kituo cha treni cha victoria kikafungwa.

Watoto ni miongoni mwa watu 22 waliouwawa. Watu wengine 59 walijeruhiwa.

Zaidi ya simu 240 za dharua zilipigwa na magari ya kubeba wagonjwa 60 na polisi 400 wakawasili.

Baada ya shambulio mamia ya watu walitumia mitandao ya kijamii kuwapa vitanda na vyumba wale waliokwama mjini.

Nani alifanya shambulizi?

Polisi wanasema kuwa mwanamume mshambuliaji wa kujitoa mhanga alilipua bomu la kutengenezewa nyumbani na kuawa katika eneo la shambulizi.

Wanachunguza ikiwa alitekeleza shambulizi hilo peke yake au ni mmoja wa mtandao mkubwa.

Ni kipi kimefanyika kwa wale waliohusika?

Waliojeruhiwa wanatibiwa katika hospitali ndani na nje ya mji wa Manchester.

Kituo cha kutoa msaada kwa yeyote ambaye anahitaji usaidizi kimebuniwa.

Serikali imejibu vipi?

Waziri mkuu Theresa May amelaamia shambulio hilo la kigaidi.

"Mawazo yetu yote yako kwa waathiriwa na kwa familia za wale waliojeruhiwa." alisema May

Pia amefanya mkutano wa dharura.

Kampeni zote za uchaguzi mkuu zimesitishwa hadi wakati usiojulikana.

Shambulizi hilo limesababisha nini?

Eneo lote la ukumbi wa Manchester na kituo cha treni cha Victoria limefungwa kwa uchunguzi.

Huduma zote za treni kutoka na kuingia kituo cha Victoria zimesitishwa

Usalama umeimarishwa ndani ya Manchester, London na kwenye vituo vya usafri kote nchini Uingereza.

Image caption Eneo la shambulio

Tunafahamu nini kuhusu uchunguzi?

Polisi wanasema kuwa uchunguzi ni mgumu na wamewashauri watu kuacha kueneza uvumi kuhusu mshambuliaji

Ikiwa mlipuko huo utathibitishwa kuwa wa kigaidi utakuwa mbaya zaidi nchini Uingereza tangu watu 52 wauawe kwenye mashambulizi ya London mwaka 2005.