'Kifaa' cha Korea Kaskazini chashambuliwa na Korea Kusini

Kifaa hicho kilirushwa katika eneo ambalo ni marufuku kwa shughuli za kijeshi Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kifaa hicho kilirushwa katika eneo ambalo ni marufuku kwa shughuli za kijeshi

Korea Kusini inasema kuwa imekishambulia ''kifaa'' kutoka Korea Kaskazini kilichorushwa katika eneo lisilo la kijeshi.

Takriban risasi 90 zilifyatuliwa zikielekezwa kwa kifaa hicho ambacho kufikia sasa hakijajulikana kilikuwa nini hasa.

Korea Kaskazini imerusha ndege zisizokuwa na rubani katika mpaka huo siku za hapo awali.

Katika taarifa, jeshi la Korea Kusini limesema kuwa jeshi lake linaweka ulinzi mkali.

Kisa hicho kinajiri wakati ambapo kuna wasiwasi mkubwa katika rasi ya Korea.

Siku ya Jumapili Pyongyang ilitekeleza kile ilichodai kuwa jaribio lililofanikiwa la kombora la masafa ya kadri.

Jaribio hilo linajiri wiki moja baada ya Korea Kaskazini kufanyia majaribio kile ilichodai kuwa ni kombora jipya linaloweza kubeba kichwa cha nyuklia, ambalo lina uwezo wa kushambulia Marekani.

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kufanya kikao cha faragha kuhusu Korea Kaskzini siku ya Jumanne jioni.

Katika taarifa siku ya Jumatatu ,lilikubali kuchukua hatua muhimu ikiwemo vikwazo ili kuishinikiza Korea Kaskazni kusitisha hatua yake .

Ongezeko hilo la wasiwasi linajiri wakati ambapo kuna rais mpya Korea Kusini .

Moon Jae alikula kiapo cha kuchukua mamlaka mapema mwezi huu baada ya mtangulizi wake Park Geun Hye kushtakiwa.

Kwa sasa anakabiliwa na mashtaka ya ufisadi.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Ndege isiokuwa na rubani iliorushwa karibu na eneo la Paju

Bwana Moon anapendelea majadiliano na Korea Kaskazini ikilinganishwa na mtangulizi wake.

Maafisa wa Korea Kusini hawakusema iwapo walikishambulia ama kukikamata kitu hicho kilichorushwa katika eneo hilo ambalo ni marufuku kwa shughuli zozote za kijeshi lakini visa kama hivyo vimetokea hapo awali.

Mnamo mwezi Januari 2016 wanajeshi waliopo mpakani mwa Korea Kusini waliishambulia ndege moja isiokuwa na rubani.

Mnamo 2014, maafisa wa Korea Kusini walisema kuwa walipata ndege mbili zisizokuwa na rubani katika eneo ambalo ni marufuku kwa shughuli za kijeshi karibu na Paju na nyengine katika kisiwa karibu na eneo linalozozaniwa la baharini kati ya mataifa hayo ya Korea.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii