Tedros Adhanom Ghebreyesus kumrithi Margaret Chan

UN Haki miliki ya picha AFP
Image caption Tedros Adhanom Ghebreyesus , mkurugenzi mpya wa WHO

Tedros Adhanom Ghebreyesus ambaye ni raia wa Ethiopia, ameteuliwa kuwa mkurugenzi mkuu wa Shirika la afya duniani (WHO).

Uteuzi huo unamfanya Tedros kuwa muafrika wa kwanza kuongoza kitengo hicho cha afya ndani ya umoja wa mataifa, baada ya kujizolea kura zote 186 za nchi wanachama.

Inaelezwa kuwa mkurugenzi huyo anamrithi mtangulizi wake Margaret Chan,ambaye anapaswa kuondoka madarakani baada ya miaka kumi ya utumishi wake ambao utafikia tamati mwezi wa sita mwaka huu.

Wakati wa utawala wake, Margareth aliwahi kushutumiwa vikali kutokana na kasi yake ndogo katika kushughulikia mlipuko wa ugonjwa wa Ebola Afrika magharibi. Kitengo hicho kiliwahi kushutumiwa kwa kukosa kuzingatia ishara muhimu za tahadhari juu ya mlipuko hatari wa ugonjwa huo ulioanza mnamo mwezi December mwaka 2013 na hatimaye kuua watu elfu kumi na mmoja.

Akihutubia mkutano wa Afya muda mfupi kabla ya upigwaji kura, Dr Tedros aliahidi kushughulikia dharula zote zitakazojitokeza kwa wakati , haraka na kwa ufanisi.Lakini pia ameahidi kusimamia haki za masikini, huku akinukuliwa akisema kwamba "juhudi zote zinapaswa kuelekezwa katika chanjo za afya . Sitapumzika mpaka hapo changamoto inayotukabili mpaka itakapokuwa imetatuliwa."

Dr Tedros ni nani?

Kwanza ana umri wa miaka 52. Ameoa , ana watoto watano na anaishi nchini Ethiopia, kazi yake kwa sasa ni Waziri wa afya na mambo ya nje , mwenyekiti wa bodi ya mfuko wa kimataifa unaoshughulika kupambana na UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria.

Wasifu wake;-

Anajulikana kimataifa kama mtafiti wa malaria akiwa na digirii ya masuala ya afya ya jamii.

Uteuzi wake katika nafasi hii mpya haukuwa rahisi, ulikuwa na vikwazo kadhaa.

Hivi karibuni ametuhumiwa kwa kugubika kesi tatu za ugonjwa wa kipindupindu nchini Ethiopia ingawa wafuasi wake wamekana tuhuma hizo.

Nacho chama kikuu cha upinzani nchini humo wanampinga Dr Thedros. Wanaishutumu pia serikali kw ukiukwaji wa haki za binaadamu na kuamini kwamba uteuzi wa Dr Tedros ni jitihada ama njama za kuipaisha hadhi ya Ethiopia kimataifa.

Wakati shutuma na changamoto hizo zikielekezwa kwake, Dr Tedros mwenyewe ameendelea kuelezea vipaumbele vyake ikiwemo haja yake kuona kila mtu anakuwa na uwezo wa kumudu gharama za afya na maisha bora, bila kujali wao ni akina nani ama wanaishi wapi.

Yeye aliwaambia wajumbe katika Baraza Kuu la afya duniani kwamba anaahidi kila siku atakuwa tayari kuleta mabadiliko na kwamba yuko tayari kutumika.

Katika nafasi yake hiyo mpya, Dr Tedros ana vipaumbele vitano ambavyo ni pamoja na ;-

- Kuendeleza chanjo ya afya wote

- Kuhakikisha WHO inajibu kwa haraka na kwa ufanisi kwenye milipuko ya magonjwa na dharura zitakazojitokeza

- Kuweka ustawi wa wanawake, watoto na vijana katika afya ya kimataifa na maendeleo ya makundi hayo

- Kusaidia mataifa kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa kwa afya

-Kuifanya WHO kuwa kitengo chenye uwazi na uwajibikaji

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii