Polisi 4 wauawa katika mlipuko Garissa Kenya

Maafisa wa usalama Garissa Haki miliki ya picha EPA
Image caption Maafisa wa usalama katika shambulio la 2015 ambapo watu 147 waliuawa katika shambulio la al Shabaab dhidi ya chuo kikuu cha Garissa Kenya

Maafisa 4 wa polisi wameuawa na wengine 4 kujeruhiwa, mmoja akiwa katika hali mahututi, katika shambulio Jumatano alfajiri eneo la Liboi kaskazini mashariki mwa Kenya karibu na mpaka na Somalia.

Duru za usalama zinaarifu kuwa gari la kijeshi lililokuwa limewabeba maafisa wa usalama wa Kenya lilikanyaga bomu la kutegwa ardhini.

Taarifa katika baadhi ya vyombo vya habari Kenya zinasema kuwa maafisa hao walikuwa wanapiga doria katika eneo la Kulan wakati gari lao lilipokanyaga bomu hilo.

Maafisa wengine watatu wamejeruhiwa katika shambulio hilo na inaarifiwa wamesafirishwa hadi mjini Nairobi kupokea matibabu maalum.

Awali katika mtandao wa kijamii Twitter - Shirika la msalaba mwekundu limesema: " gari limekanyaga bomu la ardhini na kuwajeruhi watu 8 baina ya Liboi na Kulan, kaunti ya Garissa."Liliendelea kusema kwamba linashughulikia tukio hilo.

Gazeti la Daily Nation linaripoti kuwa maafisa hao walikuwa wanasafiri kwa gari la kituo cha polisi cha Kulan katika barabara ya Liboi - Milan wakati gari hilo lilipokanyaga bomu la kutegwa ardhini.

Inaarifiwa gari hilo liliharibika vibaya.

Makamu wa rais William Ruto ametuma ujumbe katika Twitter akisema, "Waathiriwa wa shambulio la Liboi kaunti ya Garissa wamo mawazoni mwangu. Ni lazima tuujenga ukuta mpakani".

Serikali ya Kenya iliidhinisha ujenzi wa ukuta katika mpaka baina ya Kenya na Somalia kuzuia uhalifu baada ya shambulio la kigaidi dhidi ya chuo kikuu cha Garissa mnamo mwaka 2015.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii