Wanawake walivyogeuzwa watumwa wa ngono wa al-Shabab

Wanawake wa kikundi cha Salama

Wakati Salama Ali alipoanza kuchunguza kutoweka kwa ndugu zake wawili wadogo mwaka uliopita, aligundua jambo la kutamausha sana.

Sio vijana wa kiume pekee waliofunzwa itikadi kali ambao walikuwa wakihamia Somalia kujiunga na al-Shabab, bali pia wanawake walikuwa wakisafirishwa kimagendo na kufanywa watumwa wa ngono.

Habari zozote kuhusu ndugu zake Salama zilitafutwa kimya kimya tu na kwa siri, kwani ishara yoyote za uhusiano na kundi la kigaidi la al-Shabab zingepelekea vikosi vya usalama kuanza kuuliza maswali.

Hivyo alikutana kwa siri na wanawake wengine mjini Mombasa na viunga vyake, wakielezana habari zozote walizokuwa nazo na kutafuta taarifa kuhusu ndugu zao wa kiume ambao walikuwa wametoweka kwa njia za kushangaza.

"Tuligundua kuwa tulikuwa wengi sana," Salama anasema.

Lakini Salama pia aligundua kitu kingine tofauti - hadithi za wanawake ambao walikuwa wamepelekwa Somalia bila hiari yao.

Ni wanawake vijana na wazee, kutoka jamii za Kikristo na Kiislamu, kutoka Mombasa na sehemu nyingine za mkoa wa pwani ya Kenya.

Waliahidiwa kazi nzuri nzuri katika miji mingine na nchi nyingine, kisha wakatekwa nyara.

Septemba mwaka jana Salama alipata mafunzo kama mshauri na kuanzisha kikundi cha siri cha kutoa msaada kwa wanawake waliofanikiwa kutoroka.

Huwezi kusikiliza tena
Wanawake waliofanywa watumwa wa ngono wa al-Shabab

Anasema baadhi yao walifika wakiwa na watoto, wengine wakiwa wameambukizwa virusi vya Ukimwi na wengine wakiwa na magonjwa ya kiakili yaliyosababishwa na yale waliyoyapitia.

"Wanaume walikuwa wanakuja na kufanya mapenzi nami - siwezi kukuambia idadi yao," anasema mmoja, huku akitikisa kichwa. "Kwa miaka hiyo mitatu, kila mtu alikuwa anakuja kulala na mimi."

"Waliwaleta wanaume wawili au watatu kwa kila mwanamke kila usiku," anasema mwingine. "Tulikuwa tunabakwa mara kwa mara."

Kenya imeshambuliwa mara kwa mara na al-Shabab, na jeshi la Kenya linawawinda wapiganaji katika msitu wa Boni unaopakana na Somalia.

BBC imezungumza na wanawake zaidi ya 20 na wote wanasema waliwekwa katika msitu na kusafirishwa huko. Kuna uwezekano wa huo kuwa ni msitu wa Boni.

Faith ni mwanachama mmoja wa kikundi cha Salama ya aliyetoroka juzi tu.

Alikuwa na umri wa miaka 16 wakati aliahidiwa kazi mjini Malindi, kaskazini mwa mji wa Mombasa, na wazee wawili.

Kwa vile alihitaji kazi sana alipanda basi siku iliyofuata na abiria wengine 14. Wote walipewa maji yaliyokuwa na dawa za kulewesha .

"Tulipopata fahamu, kulikuwa na wanaume wawili ndani ya chumba," Faith anasema. "Walitufunga macho kwa skafu nyeusi. Walitubaka katika chumba hicho."

Alipewa dawa za kumlewesha tena na alipopata fahamu, Faith alikuwa katika sehemu moja, katikati ya msitu uliojaa giza.

Aliambia angeuawa akijaribu kutoroka.

Kwa miaka mitatu alikuwa mpishi wa wanaume wa asili ya Kisomali waliokuwa "na ndevu ndefu ndefu".

Alikuwa pia na mimba, kutokana na kubakwa, na alilazimika kujifungua peke yake msituni.

"Bibi yangu alikuwa mkunga wa jadi, hivyo nilikuwa na elimu kidogo," anasema.

Faith alisaidiwa kutoroka na mganga aliyekuwa msituni akitafuta mizizi.

Image caption Faith na mtoto wake

Mtoto wake, ambaye alizoea kukaa uchi msituni, sasa anaona vigumu kukabiliana na maisha ya mji na anapambana na usingizi usiku hadi mamake atakapomshika katika mikono yake na kukaa naye nje.

Alizoea "kuishi kama mnyama katika msitu", Faith anasema.

Sara, mke wa zamani wa mpiganaji wa al-Shabab, anasema hii sio bahati mbaya. Kuna mpango wa kuzaa kizazi kijacho cha wapiganaji, anasema, kwani ni vigumu kuwaleta watu waishi katika kambi nchini Somalia, na ni rahisi kuwapotosha watoto.

"Katika kambi yangu, kulikuwa wanawake ambao walitumwa nje kuwaleta wanawake wengine," Sarah anasema. "Wanataka tu wanawake kujifungua ili wawe wengi."

Serikali ya Kenya inakubali kuwa kuna tatizo lakini Kamishna wa jimbo la Mombasa Evans Achoki, anasema ni vigumu kujua ukubwa wa tatizo lenywe kwa sababu wanawake hawajitokezi kutoa taarifa.

Huwezi kusikiliza tena
Msitu unaotumiwa na al-Shabab kusafirisha wanawake mateka

Ingawa kuna mpango wa kutoa msamaha kwa wapiganaji wanaorudi nchini kenya kutoka Somalia, pia kuna taarifa za watu ambao wametoweka kwa ghafla, au wameuawa kwa kupigwa risasi

"Watu wanaiogopa serikali," anasema Sureya Hersi kutoka shirika lisilo la kiserikali la 'Sisters Without Borders'

"Wale walioenda huko kwa kupenda na wale waliolazimishwa wote wanaonekana kuwa na hatia."

Majina ya wanawake wote katika hadithi hii yamebadilishwa kwa ajili ya usalama wao

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii