Nyota wa Afghanistan achoma rinda lililozua utata

Bi Sayeed alivaa rinda hilo wakati wa tamasha moja huko mjini Paris Haki miliki ya picha FACEBOOK/ARYANA SAYEED
Image caption Bi Sayeed alivaa rinda hilo wakati wa tamasha moja huko mjini Paris

Mwanamuziki mmoja nchini Afghanistan amelichoma rinda lake linalofanana na ngozi yake hadharani baada ya viongozi wa dini na raia kumkosoa kwa kulivaa wakata wa tamasha moja la hivi karibuni.

Aryana Sayeed alichapisha kanda ya video katika mtandao wa facebook akionyesha rinda hilo linavyochomeka baada ya kuzua hisia Afghanistan.

Rinda hilo la kubana alilolivaa katika tamasha mjini Paris mwezi Mei tarehe13 lilishutumiwa na viongozi wa dini pamoja na mitandao ya kijamii huku watu kadhaa wakisema kuwa linakiuka utamaduni wa Aghanistan.

Hakufurahia kulichoma rinda hilo akiwaambia zaidi ya wafuasi wake milioni 1.6 kwamba ''iwapo munafikiri kwamba tatizo kubwa nchini Afghanistan ni rinda hili nitalichoma hii leo kwa sababu yenu''.

Bi Sayeed ni mtu maarufu nchini Afghanistan, akiwa mwanamuziki, mwandishi wa nyimbo, muigizaji katika runinga anayeimbia nyimbo za Hip hop na nyimbo za Afghanistan.

Pia ni mmojawapo ya majaji wa kipindi cha vipaji vya muziki kinachopeperushwa hewani na runinga ya Tolo yenye makao yake huko Kabul.