Tatizo la kompyuta latatiza safari za ndege za British Airways

Msongamano wa abiria wa kampuni ya British Airways katika uwanja wa ndege wa Heathrow
Image caption Msongamano wa abiria wa kampuni ya British Airways katika uwanja wa ndege wa Heathrow

Abiria wanaosafiri na Shirika la Ndege la British Airways, wamecheleweshwa kwa sababu ya matatizo ya kompyuta.

Baadhi ya ripoti zinaeleza kuwa matatizo hayo huenda yameathiri shughuli za shirika hilo dunia nzima.

BA imeomba msamaha katika mitandao ya jamii, na inasema inajaribu kumaliza tatizo hilo haraka iwezekanavyo.

Tatizo hilo linamaanisha kwamba baadhi ya tovuti za kampuni hiyo ya ndege haipatikani na kwamba baadhi ya abiria wanasema kwamba hawawezi kuingia katika tovuti hiyo kwa kutumia simu.

Image caption Uwanja wa ndege wa Heathrow nchini Uingereza

Ndege za kampuni hiyo zinazotua katika uwanja wa Heathrow mjini London haziwezi kuegeshwa kwa kuwa ndege zinazoondoka haziwezi kutoka katika lango kuu, hali iliowafanya abiria kukwama katika ndege.

Mwandishi Martyn Kent alisema kuwa amekuwa ndani ya ndege katika uwanja wa Heathrow kwa dakika 90.

Anasema kwamba rubani wa ndege aliambia abiria kwamba tatizo hilo la kompyuta ni 'janga'.

Uwanja wa ndege wa Heathrow umewashauri abiria kuangalia muda wa safari zao kabla ya kuelekea katika uwanja huo.

Mada zinazohusiana