Madai ya mipango ya Rais Zuma kuhamia Dubai yaibuka Afrika Kusini

Je, Rais Zuma ana mipango ya kuhamia Dubai? Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Je, Rais Zuma ana mipango ya kuhamia Dubai?

Nchini Afrika kusini kashfa mpya inatokota inayozingira madai ya rais Jacob Zuma ya kuzingatia kuhamia Dubai.

Barua pepe hizo zimechapishwa na gazeti moja nchini Afrika kusini na zinaonyesha uhusiano mkubwa kati ya rais wa Afrika kuisni Jacob Zuma na familia yenye utata, Gupta, hususan kuhusu madai kwamba rais Zuma anazingatia kuhamia Dubai.

Wakati chama tawala nchini Afrika Kusini ANC kinakumbwa na vita vya ndani kwa ndani, barua pepe hizo zinatarajiwa kuibua mjadala mkali kwani zinafichua mipango ya rais Zuma ya kuhamia Dubai.

Barua pepe hizo baina ya mwanawe Zuma, Duduzane, na vigogo wa kampuni inayomilikiwa na familia tatanishi ya Gupta, zinashirikisha barua moja iliyotumwa kwa familia ya kifalme nchini Dubai, ambapo Zuma anasema angetaka kuwa na makao ya pili huko Dubai.

Madai hayo yanaibua mjadala wa iwapo rais Zuma anajiandaa kubwaga manyanga kwani chama cha ANC kinaonekana kumgeuka.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Zuma amekumbwa na kashfa nyingi ikiwemo ya makao ya Nkandla

Msemaji wa rais amepuuza barua pepe hizo kama uvumi na uchokozi.

Hayo yakiarifiwa, ombi la kutokuwa na imani na rais Jacob Zuma limewasilishwa kwa kamati kuu ya chama cha ANC inayokongamana mjini Pretoria.

Ni mara ya pili sasa ambapo waasi wa chama hicho wanawasilisha ombi hilo.

Hata hivyo, huenda wanchama wa kamati hiyo watiifu kwa rais Zuma wakaangusha mswada huo.

Kwa sasa kesi inaendelea katika mahakama ya kikatiba ya iwapo wabunge wa Afrika kusini watapiga kura ya siri ya kwa mswada wa kutokuwa na imani na rais Jacob Zuma.

Kamati hiyo inatarajiwa kuamua atakayemridhi bwana zuma mwezi Desemba.