Meya wa Paris 'kupiga marufuku' tamasha la watu weusi

Kibonzo hiki kimepakiwa na waandalizi wa tamasha hilo mtandaoni Haki miliki ya picha Nyansapo Festival
Image caption Kibonzo hiki kimepakiwa na waandalizi wa tamasha hilo mtandaoni

Meya wa mji wa Paris nchini Ufaransa ameomba tamasha ya wanawake weusi katika mji huo lipigwe marufuku kwa sababu Wazungu hawaruhusiwi kuhudhuria.

Tamasha hilo la Nyansapo litakalofanyika mwezi Julai limekuwa likiuzwa kama la "wanawake weusi".

Asilimia 80 ya nafasi katika tamasha hilo imetengewa wanawake weusi.

Watu weusi wa jinsia zote wataruhusiwa kuingia sehemu nyingine, kisha kutakuwa na sehemu ya tatu ambao watu wa asili zote wataruhusiwa kuingia.

Anne Hidalgo aliandika kwenye Twitter kwamba ana haki ya "kuwafungulia mashtaka waandalizi wa tamasha hilo kwa kosa la kufanya ubaguzi".

Baadhi ya mashirika ya kupinga ubaguzi wa rangi nchini Ufaransa yameshutumu tamasha hilo.

SOS Racisme walisema tamasha hilo ni "laana" na kwamba linaendeleza "kutenganishwa kwa watu wa asili mbalimbali."

Ijumaa, kiongozi wa kanda wa chama cha mrengo wa kulia National Front alimtaka Bi Hiladlgo aeleze ni kwa nini hafla hiyo ya "ubaguzi wazi wa rangi" inafanyika.

Waandalizi hata hivyo wamejitetea kupitia taarifa na kusema kwamba wameponza na kampeni ya kuwapotosha watu ambayo imeendelezwa na watu wa mrengo wa kulia.

Wamesema wanasikitishwa sana na hali kwamba baadhi ya mashirika yanayopinga ubaguzi wa rangi yameshawishika.

Tamasha hilo litafanyika katika eneo ambalo linamilikiwa na baraza la mji wa Paris, lakini hafla yenyewe haiko wazi kwa watu wote.

Waandalizi wamesema meya huyo hana mamlaka yoyote ya kuingilia hafla hiyo.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii