Mgombea urais adaiwa kutaka kujirusha kutoka kwenye ghorofa Kenya

Baadhi ya wanaume wakisajiliwa kama wapiga kura nchini Kenya kufuatia kuanzishwa kwa shughuli hiyo siku ya Jumatatu
Image caption Raia wakijisajili kuwa wapiga kura nchini Kenya awali. Uchaguzi mkuu utafanyika Agosti 8

Mmoja wa waliojitokeza kugombea urais katika uchaguzi mkuu mwezi Agosti nchini Kenya alijaribu kujirusha kutoka jumba la ghorofa, taarifa katika vyombo vya habari nchini humo zinasema.

Bw Peter Solomon Gichira anadaiwa kujaribu kujirusha kutoka ghorofa ya sita katika afisi za Tume Huru ya Uchaguzi (IEBC) jijini Nairobi baada ya ombi lake la kutaka kuwania urais kukataliwa Jumamosi jioni.

Mkuu wa polisi wa Nairobi Japheth Koome amesema Bw Gichira atafunguliwa mashtaka ya kuzua fujo eneo la umma, kuharibu mali na kujaribu kujitoa uhai.

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation, mkuu wa polisi wa kituo cha Central Robinson Thuku alisema Bw Gichira alikuwa ameenda afisi za IEBC kufuatilia ombi lake alipofahamishwa kwamba ombi lake lilikataliwa.

Ni hapo ambapo alianza kulalamika na akavunja dirisha na kujaribu kuruka nje lakini akazuiwa na maafisa wawili ambao pia walimkamata.

Bw Thuku alisema mwanasiasa huyo atafikishwa mahakamani Jumatatu.

Polisi walikataa kumwachilia dhamana na kusema wanamzuilia kwa ajili ya usalama wake.

Mgombea mwenza wa Bw Gichira, Kelly Watima, hata hivyo alisema mwenzake amekuwa akihangaishwa tangu alipotangaza nia ya kutaka kuwania urais.

"Bw Gichira amekuwa akihangaishwa na maafisa wa IEBC na sasa polisi wanamzuilia ndipo akose fursa ya kuwasilisha karatasi zake za uteusi …mbona wanamuogopa…je, ni kwa sababu ni tishio kwao?" alisema, kwa mujibu wa Daily Nation.

Bw Gichira ni miongoni mwa wanasiasa kumi waliokuwa wameeleza nia ya kutaka kuwania urais lakini wakakosa kuidhinishwa na tume hiyo kwa kukosa kutimiza amsharti mbalimbali.

Kuna wagombea kumi walioidhinishwa, ambao wamekuwa wakiwasilisha karatasi zao Jumapili na leo Jumatatu.

Miongoni mwa waliofanikiwa kuwasilisha karatasi zao Jumapili ni aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga, mgombea huru Ekuru Aukot na Abdouba Dida ambaye pia aliwania urais mwaka 2013.

Waliopangiwa kuwasilisha karatasi zao za uteuzi leo ni pamoja na Rais Uhuru Kenyatta ambaye anawania kwa mara ya pili.

Mada zinazohusiana