Angola yathibitisha rais wake apata matibabu Hispania.

dos
Image caption Rais Jose Eduardo dos Santos

Kwa mara ya kwanza, serikali ya Angola imethibitisha kuwa rais Jose Eduardo dos Santos yuko nchini Hispania kwa ajili ya matibabu.

Dos Santos aliondoka Angola mwanzoni mwa mwezi wa tano.

Kulikuwa na tetesi kuwa rais huyo alikuwa huko Hispania kitu ambacho mtoto wake wa kike, Isabel alikana taarifa hiyo.

Waziri wa mambo ya nje, George Chikoti aliiambia Radio ya Ufaransa, RFI sehemu ambayo rais Dos Santos aliko na kueleza taarifa fupi juu ya hali ya ugonjwa wa rais huyo.

''Rais Dos Santos yuko Hispania na anaendelea vizuri hivyo atarejejea,'' Chikoti alisema.

Waziri huyo aliongeza kusema kuwa rais Dos Santos huwa anaenda Hispania kila mara kwa ajili ya kufanya vipimo vya afya yake hivyo hilo ni jambo la kawaida kabisa.

Rais wa Angola ambaye ana umri wa miaka 74, amekuwa madarakani kwa miaka 38 ingawa sasa anatarajia kuachia ngazi mara baada ya uchaguzi utakaofanyika mwezi Agosti mwaka huu.

Mada zinazohusiana