Mwanamume aliyewachoma kisu wageni Zanzibar asakwa

Visiwa vya Zanzibar hutegemea sana utalii Haki miliki ya picha PA
Image caption Visiwa vya Zanzibar hutegemea sana utalii

Polisi visiwani Zanzibar wanamsaka mwanamume mmoja anayedaiwa kuwachoma kwa kisu watu sita wakiwemo raia wanne wa kigeni na kuwajeruhi vibaya usiku wa kuamkia Jumatatu.

Mwanamume huyo aliwashambulia wageni hao katika mgahawa wa Lukman Mkunazi Mjini Zanzibar.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Hassan Nassir Ali aliwaambia waandishi wa habari Jumatatu kuwa mtuhumiwa aliyetenda hayo hayatambuliwa kwa jina.

Hata hivyo, anafahamika kwa sura na, anakisiwa kuwa na umri wa miaka 25.

Bw Ali alisema uchunguzi wa awali umebaini mtuhumiwa huyo alifika katika mgahawa huo na kuwachoma watu watatu ambao walikuwa mgahawani hapo kwa ajili ya kujipatia chakula na kisha akakimbia na akiwa njiani akawashambulia wengine watatu.

Walioshambuliwa ni Mauget Gerarol ambaye ni raia wa Ufaransa, Liying Liang raia wa Canada na Jennifer Wolf na Anna Catharina ambao ni raia wa Ujerumani.

Wengine ni Hassan Abdallah na Sajad Hussein.

Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi, Bw Ali alisema majeruhi wote walipatiwa matibabu na kuruhusiwa lakini Mauget Gerarol raia wa Ufaransa bado amelazwa hospitalini.

Zanzibar hutegemea sana utalii.

Mada zinazohusiana