Wanajeshi washtakiwa, Sudan kusini

Ramani ya Sudan kusini
Image caption Ramani ya Sudan kusini

Mahakama ya kijeshi nchini Sudan kusini imewafungulia mashtaka wanajeshi 13, kwa makosa ya ubakaji wafanyakazi wa misaada wa kigeni na kumuua mwandishi wa habari nchini humo.

Kwa mujibu wa shirika la Habari la AFP, watuhumiwa wao walifikishwa mahakamani wakiwa na sare za aina tofauti, hali inayoonesha kuwa wanatoka vitengo tofauti, ikiwemo wanne kutoka katika kikosi kinachomlinda Rais.

Msemaji wa jeshi Abubakr Mohamed amesema wanajeshi hao pia wanakabiliwa na makosa ya uporaji na kuharibu mali.

Uchunguzi dhidi yao umekuwa ukiendelea muda mrefu.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption madhara ya vita, Sudan kusini

Nalo, Shirika la Habari la Human Right Watch limearifu kuwa, Julai 11 mwaka uliopita, majeshi ya serikali yalivamia majengo, yaliyokuwa yakikaliwa na wafanyakazi wa mashirika ya kigeni, wapatao 50.

Shirika hilo limedai kuwa wanajeshi walimuua mwandishi wa habari, kuwabaka wafanyakazi wa mashirika na kuharibu mali.

Wanajeshi hao wanadaiwa kuumua mwandishi wa habari kutokana na kabila lake.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe Sudan kusini vilianza mwezi June mwaka uliopita baada ya Rais wa nchi hiyo Salva Kiir kumshtumu makamu wake Riek Machar kuwa anapanga kumpindua.