Mcheshi aomba msamaha kwa picha ya 'kichwa cha Trump kilichokatwa'

Kathy Griffin amekuwa mkosoaji mkubwa wa utawala wa Trump Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Kathy Griffin amekuwa mkosoaji mkubwa wa utawala wa Trump

Mcheshi mmoja nchini Marekani ameomba msamaha kuhusu picha ambayo alionekana amebeba kichwa kilichokatwa kinachofanana na Donald Trump .

Katika ujumbe wa kanda ya video iliochapishwa katika mtandao wa Twitter Kathy Griffin aliomba kusamehewa na kusema kuwa alikuwa amepita mpaka.

Alisema kuwa alimuomba mpiga picha wa watu maarufu Tyler Shield kuondoa picha hiyo katika mtandao.

Picha hiyo ya kutisha ilizua pingamizi katika mitandao ya kijamii ikiwemo kutoka kwa mwana wa Trump Donald Trump Jr.

''Inatatiza lakini sio ajabu'' ,alituma ujumbe katika mtandao wa Twitter, ''hivi ndivyo ubaya wa siku hizi, wanachukulia hili kuwa sawa''.

Mwana wa aliyekuwa mpinzani wa Trump katika uchaguzi wa Marekani Hillary Clinton, Chelsea alishutumu picha hiyo akisema kuwa inaonyesha unyonge na makosa.

''Sio vizuri kufanyia mzaha wa kumuua rais'', alituma ujumbe katika mtandao wa Twitter.

Aliyekuwa mgombea wa tiketi ya urais wa chama cha Republican Mitt Romney pia naye alituma ujumbe katika mtandao wa Twitter akisema: Siasa zetu zimekosa mwelekeo lakini chapisho hilo la Kathy Griffins linaonyesha uchafu uliopo na makosa makubwa tunayofanya.

Mshindi huyo wa tuzo la uigizaji la Emmy na mcheshi amekuwa mkosoaji mkubwa wa utawala wa Trump.

Katika kanda ya video akiomba msamaha ,alisema: Sasa naona ukweli wa picha hizo.Mimi ni mcheshi lakini nilipita mipaka. Picha hizo zinakera.Ninaelewa vile zinavyowaathiri raia.Hazina tena ucheshi.naomba msamaha.

Mada zinazohusiana