Waandamanaji wataka mwanaharakati kuachiliwa Morocco

Waandamanaji nchini Morocco Haki miliki ya picha AFP
Image caption Waandamanaji nchini Morocco

Maelfu ya watu wameandamana kazkazini mwa mji wa Morocco wa Al -Hoceima wakitaka kuachiliwa huru kwa mwanaharakati maarufu.

Ripoti zinasema kuwa maafisa wa polisi wa kukabiliana na ghasia walikabiliana na waandamanaji hao kabla ya ya kusalimu amri.

Waandamanaji walianzisha pingamizi hiyo baada ya Nasser Zefzafi kukamatwa siku ya Jumatatu akishtakiwa kwa kutishia usalama wa taifa.

Bwana Zefzafi ameandaa maandamano ya miezi kadhaa dhidi ya ukosefu wa ajira na ufisadi.

Morocco imekumbwa na maandamano tangu kifo cha mvuvi mmoja katika eneo la Al-Hoceima mnamo mwezi Oktoba.

Kulingana na kituo cha habari cha AFP,waandamanaji waliokuwa wakiimba ''Sote ni Zefzafi'' walijaa katika barabara za mji wa Al-Hoceima siku ya Jumanne jioni na maafisa wa kukabiliana na ghasia walipelekwa katika eneo hilo ili kuwazuia.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mwanaharakati Zefzafi

Makabiliano yalianza lakini maafisa wa polisi wakasalimu amri bila kisa chochote.

Maandamano pia yamefanyika mjini Casablanca na katika mji mkuu wa Rabat kulingana na AFP.

Maandamano hayo yalisababishwa mwezi Oktoba iliopita na kifo cha mvuvi Moucine Fikri aliyegongwa hadi kufa na lori la kubeba taka alipojaribu kuokoa mali yake ambayo ilikuwa imechukuliwa na polisi.

Kifo chake kinafananishwa na kile cha muuza matunda wa Tunisia mwaka 2010 ambacho kilisababisha mapinduzi ya Arab Spring.