Ufilipino: Watu 36 wafariki chumba cha kamari Manila

Manila, Philippines 2 June 2017. Haki miliki ya picha EPA
Image caption Kituo cha kamari cha Resorts World Manila kimewekwa chini ya ulinzi mkali baada ya kisa hicho

Watu 36 wameuawa katika kituo cha kuchezea kamari mjini Manila, Ufilipino baada ya mtu mwenye silaha kuanza kuwafyatulia risasi watu waliokuwemo humo.

Wengi wa waliofariki inaaminika wamefariki kutokana na kukosa hewa safi kutokana na moshi uliotanda mwanamume huyo alipowasha moto meza za chumba hicho cha kamari.

Mwanamume huyo alianza kwa kupiga risasi skrini za TV katika chumba hicho cha Resorts World Manila mapema Ijumaa.

Polisi wanasema baadaye alijiteketeza.

Kisa hicho kimesababisha kuanzishwa kwa operesheni kali ya kiusalama.

Maafisa awali walisema hakuna aliyekwua ameumia kutokana na kisa hicho, lakini sasa inabainika kwamba wamepataa miili ya watu wakikagua chumba hicho.

Polisi wanasema kisa hicho kinaonekana kuwa kisa cha kawaida tu cha wizi, na kwamba hakikuhusiana na ugaidi.

Watu zaidi ya 50 wamepelekewa hospitalini wakiuguza majeraha.

Haki miliki ya picha Philippine Police
Image caption Mwanamume huyo alionekana kwenye kamera za CCTV ndani ya chumba hicho

Shambulio lilitekelezwa vipi?

Maafisa wanasema mwanamume huyo, ambaye jina lake halijatajwa kufikia sasa, aliingia ukumbi wa kituo hicho na kuanza kufyatulia risasi skrini za runinga mwendo wa saa sita usiku. Watu waliokuwemo ndani walianza kukimbia.

Pia alichoma moto meza za kamari na kujaza mkoba wake na vipande vya kuchezea kamari vya thamani ya peso milioni 113 za Ufilipino (£1.7m, $2.3m).

Baadaye alikimbia na kuingia upande wa kituo hicho wenye hoteli, akaacha mkoba wake, na kuingia chumba cha hoteli.

"Humo, alilala kitandani, akajifunika kwa blanketi aliyokuwa ameimwagilia mafuta ya petroli na kisha akajiwasha moto," mkuu wa polisi wa taifa Ronald Dela Rosa alisema Ijumaa.

Resorts World Manila wamesema katika taarifa kwamba alijipiga risasi kabla ya kujiwasha moto, na kwamba alipatikana akiwa amefariki mwendo wa saa moja asubuhi saa za Ufilipino.

Maafisa wanasema taarifa zinaonesha mwanamume huyo alikuwa na matatizo ya kiakili.

Mada zinazohusiana