Rais wa Uganda aagiza uchunguzi wa pembe za ndovu zilizotoweka

Pembe za ndovu zilizokamtwa zikichomwa moto
Maelezo ya picha,

Uganda ni njia maarufu kwa biashara haramu ya pembe za ndovu

Rais wa Uganda Yoweri Museveni ameamrisha uchunguzi mpya ufanywe ili kubaini ni vipi pembe zilizokuwa zimefichwa katika vyumba vya siri vya serikali vyenye ulinzi mkalizilivyo toweka.

Takriban tani 1.3 za pembe za ndovu zilipotea kutoka mamlaka ya wanyamapori nchini humo mwezi Novemba 2014.

Bwana Museveni alisema kuwa kuna uwezekano kwamba mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya wanyamapori Andrew Segguya alihusika na utowekaji wa pembe hizo za ndovu.

Hata hivyo bwana Segguya amekana madai hayo akisema kuwa aliidhinisha uchunguzi baada ya pembe hizo kupotea.

Rais pia amewalaumu wanadiplomasia wawili kutoka Uchina kuhusika na usafirishaji wa pembe - madai ambayo China imekana.

Msemaji wa shirika la kupambana na ufisadi nchini Uganda alisema kuwa wawili hao ambao ni maafisa katika ubalozi wa Uchina wanashukiwa kusaidia kusafirisha pembe hizo kutoka Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Jamuhuri ya Afrika ya Kati, na Sudan Kusini, kwa kuipitishia Uganda.

China imekana madai hayo ikisema kuwa hayana msingi wowote.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Uchina Hua Chunying aliwaambia wanahabari kuwa wana masharti na sheria kali kwa maafisa wa serikali yao, wafanyakazi wa ubalozi, na makundi yanayowatembelea ili kuwakanya kununua au kushiriki katika biashara za magendo.

Aliongeza kuwa ikiwa madai hayo yatathibitishwa, basi wawili hao wataadhibiwa.

Disemba mwaka jana, China ilitangaza kuwa itapiga marufuku biashara yeyote ya pembe ifikapo mwisho wa mwaka wa 2017.

Pembe ni ishara ya hadhi nchini Uchina na inauzwa takriban £852 ($1,100) kwa kilo.

Uganda ni njia maarufu inayotumiwa na wafanyabiashara kupenyeza kimagendo pembe za ndovu na vifaru kutoka Afrika, ambazo bado zinatumiwa katika baadhi ya dawa za kitamaduni za Wachina.

Kumekuwa na ongezeko la uwindaji kinyume cha sheria katika miaka ya hivi karibuni, huku ndovu 35,000 wakiuwawa katika nchi tofauti barani Afrika.