Magufuli: Anna Mghwira ana uwezo wa kuwatumikia wananchi

Bi Mghwira aliwania urais mwaka 2015 kupitia chama cha ACT Wazalendo Haki miliki ya picha Ikulu, Tanzania
Image caption Bi Mghwira aliwania urais mwaka 2015 kupitia chama cha ACT Wazalendo

Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli amemuapisha aliyekuwa mgombea urais mwaka 2015 Bi Anna Elisha Mghwira kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro na kusema anaweza kuitekeleza kazi hiyo.

Bi Anna Elisha Mghwira amejaza nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Saidi Meck Sadiki aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo ambaye aliacha kazi.

Akizungumza baada ya kumuapisha, Rais Magufuli amemtaka Bibi Anna Elisha Mghwira kwenda kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa na kuondoa kero zinazowakabili wananchi wa Kilimanjaro bila kujali itikadi za vyama vyao vya siasa, dini, makabila na kanda wanazotoka.

Alisema anaamini mwanasiasa huyo ana uwezo wa kutekeleza majukumu yanayoambatana na kazi hiyo.

"Mimi huwa siteui watu hivi hivi, huwa naangalia uwezo wa mtu, na wewe nimekuchunguza na nimejiridhisha kuwa una uwezo wa kuwatumikia wananchi, nenda kachape kazi, kawaondolee kero wananchi wa Kilimanjaro, wapo watu watakaokusema na wengine watakuonea wivu, wewe kachape kazi," amesema Dkt Magufuli, baada ya kumuapisha katika Ikulu jijini Dar es Salaam.

Bi Mghwira amemshukuru Rais kwa kumuamini na kumteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro na amemuahidi kuwa yupo tayari kwenda kufanya kazi ya kuwatumikia wananchi na kujenga Taifa.

"Ninasema hii ni heshima kwa Taifa letu, ni heshima kwa umoja wa nchi yetu, ni heshima kwa siasa za umoja wa nchi yetu, kumekuwa na minong'ono mingi sana kuwa Rais analeta nini, kuteua watu wanaitwa wapinzani, mimi sio mpinzani wa maendeleo" amesema Bi Mghwira.

Bi Mghwira alikuwa mgombea pekee wa kike wakati wa kinyang'anyiro cha urais mwaka 2015.

Amekuwa mwenyekiti wa chama cha ACT Wazalendo, chama kichanga zaidi Tanzania kilichoundwa 2014.

Mghwira, 56, anatoka mkoa wa Singida. Babake alikuwa diwani na kiongozi chama cha Tanu na baadaye CCM.

Mada zinazohusiana