Mwanamke ashtakiwa kwa ujumbe wa rununu 'zilizopelekea mpenziwe kujiua'

Haki miliki ya picha WCVB
Image caption Michelle Carter mwenye umri wa miaka 20, akiwa katika mahakama ya watoto

Mwanamke mmoja Mmarekani mwenye umri wa miaka 20, ambaye mpenziwe alijitoa uhai takriban miaka mitatu iliyopita, amepelekwa mahakamani na kushtakiwa kwa madai kuwa alimhimiza ajiue.

Michelle Carter ameshtakiwa kwa kushiriki katika kifo cha Conrad Roy wa III.

Waendesha mashtaka wanadai kuwa Bi Carter alimshawishi kijana huyo wa miaka 18 kujitoa uhai ili kupata huruma.

Amemuomba jaji kutoa uamuzi kwa kesi yake kuliko kutegemea baraza la waamuzi wa rika lake.

"Unafaa kuitimiza, Conrad, "Bi carter alimtumia ujumbe wa simu asubuhi ya Julai 2014, kulingana na rekodi iliyowasilishwa na wakili a Wilaya ya Bristol.

"Uko tayari. kilichosalia ni uwashe jenereta na utakuwa huru na mwenye furaha", aliandika.

Haki miliki ya picha WCVB
Image caption Bwana Roy alitarajiwa kuingia katika chuo kikuu baadaye mwakani

Alimwambia kwa ujumbe mwingine: "Hatimaye utakuwa na furaha ukiwa mbinguni. Hautakuwa na uchungu tena. Ni sawa kuogopa na ni kawaida. Umekaribia kufa", alipojaribu kumtia shime, aliendelea kumsukuma.

"Nilidhania unataka kufanya hivyo, wakati umewadia na uko tayari..... fanya tu mpenzi," alisema.

"Hakuna kungoja tena," aliendelea

Bwana Roy alipatikana amefariki kutokana na sumu ya kaboni monoksidi ndani ya gari lake katika egesho la magari, Massachusetts, tarehe 13 Julai 2014.

Juumbe hizo za simu ya mkononi zinamuonyesha akikataa kutimiza malengo yake ya kujiua na kwa wakati mmoja alitoka kwenye gari lake.

Mahakam ilisikia kwamba Bi Carter, ambaye alikuwa na umri wa miaka 17 wakati huo, alimshurutisha arudi ndani ya gari.

Baada ya kifo chake, aliongoza mchango wa kujulisha watu kuhusu afya ya kiakili kwa ukumbusho wake.

Haki miliki ya picha FACEBOOK
Image caption Bi Carter anasemekana kumtumia Roy ujumbe mfupi wa simu akimwambia kuwa wazazi wake watasahau kifo chake

Mamake Roy, Lynn Roy, aliambia mahakama siku ya Jumanne kuwa, hakuwa na onyo kuhusu kujiua kwa mwanawe"

Alisema kuwa alidhani alikuwa na huzuni kidogo.

Siku ya kifo chake, Bwana Roy alienda kando ya ufuo wa bahari mjini Westport, Massachusetts, akiwa na mamake na dada zake, kulingana na waendesha mashtaka.

Aliwanunulia dadazake aiskrimu, akawatania kuhusu mavazi ya kuogelea na akaongea kuhusu udhamini wa masomo aliyokuwa ameshinda, huku akitengeneza mipango mingine ya siku za usoni.

Bi Carter alimtumia mamake Roy ujumbe mfupi, baada ya kifo cha mwanawe, akimwambia kuwa roho yake ingali inaishi.

Ujumbe mmoja ulisema: "Nilimpenda, Lynn. Najua ningali kijana, lakini niliona nikiwa naye milele."

Mawakili waliomba kesi itupiliwe mbali kwa msingi ya kuwa na uhuru wa kuongea.

Lakini jaji wa mahakama ya watoto ilitoa uamuzi kuwa, swala la kumshinikiza mtu kujiua, haijalindwa katika katiba ya Marekani.