Qatar yaapa kutosalimu amri mzozo wake na nchi za Kiarabu

Doha, Qatar, June 7, 2017 Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Saudi Arabia na nchi nyingine kadha za Kiarabu zimesitisha safari za ndege kuingia na kuondoka Qatar

Qatar imeapa kwamba haitasalimu amri katika mzozo wake kuhusu sera yake ya kigeni na nchi nyingine za Kiarabu huku shirika la habari la Al Jazeera likivamiwa na wadukuzi.

Nchi hizo zinaituhumu Qatar kuwa inaunga mkono makundi ya kigaidi na makundi yenye msimamo mkali.

Waziri wa mambo ya nje wa Qatar Sheikh Mohammed bin Abdulrahman al-Thani amesema anaunga mkono zaidi kutumiwa kwa demokrasia kutatua mzozo huo na kwamba hakuwezi kuwa na suluhu inayoweza kupatikana kupitia nguvu za kijeshi, ameambia Reuters.

Qatar imepuuzilia mbali tuhuma hizo kwamba inaunga mkono makundi ya Kiislamu yenye msimamo mkali.

Hayo yakijiri, shirika la habari la Al Jazeera kutoka Qatar limesema kwamba limeshambuliwa na wadukuzi.

"Mtandao wa habari wa Al Jazeera umevamiwa na wadukuzi mtandaoni katika mifumo yake yote, kwenye tovuti na mitandao ya kijamii," Al Jazeera wameandika kwenye Twitter.

Shirika hilo limehusishwa kwenye mzozo huo wa sasa, na nchi nyingine za Ghuba zilifungia shirika hilo la habari Mei.

Kwenye tovuti yake, shirika hilo limesema huduma zake zote zinafanya kazi kama kawaida lakini mashambulio hayo ya wadukuzi "yanaongezeka kasi na ni ya aina nyingi."

Saudi Arabia na nchi nyingine kadha za Kiarabu zilikatiza safari na uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo na Qatar Jumatatu.

Emir wa Kuwait amekuwa akijaribu kufanikisha mashauriano kati ya Qatar, Saudi Arabia na Umoja wa Milki za Kiarabu (UAE).

Akiongea na wanahabari mjini Dohar Alhamisi, Sheikh Mohammed alisema Qatar imetengwa "kwa sababu tumefanikiwa na tunaangazia kupiga hatua mbele."

"Sisi ni jukwaa la amani na si ugaidi. Mzozo huu unatishia uthabiti wa kanda yote," alisema, na kuongeza.

"Hatuko tayari kusalimu amri, hatutasalimu amri, hatutaacha uhuru wa sera yetu ya kigeni."

Amesema Iran imejitolea bandari zake tatu zitumiwe na meli kusafirisha maji na chakula kwa Qatar, lakini Qatar bado haijakubali rasmi msaada huo.

Qatar hutegemea sana mataifa ya nje kwa chakula na mzozo wa sasa umesababisha watu kukimbia kulimbikiza hazina ya chakula. Kumeshuhudiwa uhaba wa chakula katika baadhi ya maeneo.

Sheikh Mohammed amesema Qatar haijawahi kukubana na uadui kama wa sasa.

Kwingineko, Urusi imesema Sheikh Mohammed atasafiri Moscow kwa mazungumzo na mwenzake wa urusi, Sergei Lavrov, Jumamosi.

Watazungumzia "masuala ya dharura ya kimataifa" shirika la habari la Tass liliripoti lakini halikutoa maelezo zaidi.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii