Papa Francis awataka makasisi Nigeria wamtii la sivyo watimuliwe

Pope Francis Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Papa Francis amewapa makasisi hao hadi tarehe 9 Julai waandike barua wakiahidi kumtii na waombe msamaha.

Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani Papa Francis amelitaka kundi la mapadri nchini Nigeria waahidi kumtii na kuheshimu uamuzi wake la sivyo wafukuzwe kutoka kwenye kanisa hilo.

Amesema hayo kutokana na hatua ya makasisi katika jimbo la Ahiara kumkataa askofu aliyeteuliwa mwaka 2012.

Papa aliwaambia waumini wa kanisa hilo kutoka Nigeria waliokuwa Roma wiki iliyopita kwamba "watu wa Mungu wameshangazwa sana" na yaliyotokea.

Ni nadra sana kwa Papa kutoa vitisho vya aina hiyo, anasema mwandishi wa BBC wa masuala ya kidini Martin Bashir.

Amewapa makasisi hao hadi tarehe 9 Julai waandike barua wakiahidi kumtii na waombe msamaha.

Rais wa Chama cha Maaskofu wa Nigeria, Akofu Mkuu Ignatius Kaigama, alikuwa katika mkutano hao mjini Roma na aliambia BBC kwamba Papa Francis alikuwa amesikitishwa sana na yale yalitokuwa yakitokea na kwamba ungeona "uchungu kwenye macho yake."

Haki miliki ya picha Aid to the Church in Need
Image caption Askofu mkuu Ignatius Kaigama amesema Papa alionekana wazi kwamba alikuwa amekereka

"Alikuwa amekereka wkamba watoto wake wanaelekea njia tofauti," aliongeza askofu mkuu huyo.

Tangu Askofu Peter Okpaleke alipoteuliwa na mtangulzii wa Papa wa sasa, Benedict XVI, Askofu mkuu Kaigama amekuwa kwenye kundi la viongozi wa kidini ambao wamekuwa wakijaribu kuwashawishi makasisi Ahiara, kaskazini mashariki mwa Nigeria wakubali uteuzi wake.

Aliambia BBC kwamba tatizo kuu ni kuwa makasisi hao na askofu huyo wanatoka ukoo tofauti wa kabisa la Igbo.

Aliongeza kuwa makasisi hao walishangaa ni vipi mtu kutoka nje ya jimbo hilo la kanisa aliteuliwa ilhali kuna mmoja wao ambaye alikuwa amehitimu.

Mwaka 2012, makasisi hao walifanya maandamano na kuwasilisha maombi rasmi wakitaka askofu kutoka eneo lao ateuliwe.

Kuomba 'Mungu aingilie kati'

Lakini Askofu mkuu Kaigama amesema "Kanisa Katoliki limekuwa likiendesha shughuli zake hivi kwa miaka mingi na hilo halitabadilika sasa kwa sababu wanataka mtu kutoka eneo lao.

"Papa anahitaji utiifu kamili."

Jimbo la Ahiara linapatikana Mbaise, eneo lenye Wakatoliki wengi katika Jimbo la Imo, ilhali Askofu Okpaleke anatoka jimbo jirani la Anambra.

Haijabainika iwapo makasisi hao wamejibu makataa hayo ya Papa.

Lakini Askofu Mkuu Kaigama amesema yeye na Wakatoliki wengine wa Nigeria wanaomba "Mungu aingilie kati" na suluhu ipatikane.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii