Wagombea urais wawasilisha nyaraka Rwanda

Dkt Frank Habineza alipokuwa anawasilisha nyaraka zake za kuwania urais
Image caption Dkt Frank Habineza alipokuwa anawasilisha nyaraka zake za kuwania urais

Wakati uchaguzi wa urais ukikaribia nchini Rwanda, wagombea wameanza kuwasilisha nyaraka zao kwa tume ya uchaguzi.

Kiongozi wa chama cha Green Dr Frank Habineza amekuwa wa kwanza kuwasilisha rasmi kwa tume ya uchaguzi nyaraka za kumwezesha kugombea kiti cha urais kwa tiketi ya chama hicho.

Dkt Habineza ametangaza kuwa chama chake kinataka mabadiliko akisisitiza kuwa ndicho pekee kilichopinga rais Kagame kuongezewa muhula wa tatu.

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Kalisa Mbanda amethibitisha kupokea rasmi nyaraka za mgombea wa kiti cha urais kwa tiketi ya chama cha Green Dkt Frank Habineza.

Nyaraka hizo ni pamoja na hati ya kuzaliwa, ya uraia na uthibitisho wa kuwa hajafungwa jela kwa miezi 6.

Mwandishi wa BBC Yves Bucyana anasema mgombea anatakiwa pia kuthibitisha kuwa hana uraia wa nchi nyingine.

Dkt Frank Habineza ambaye alikuwa na uraia wa nchi ya Sweden ameonyesha karatasi ya kuthibitisha kuwa tayari alirejesha uraia huo.

Baada ya kukabidhi nyaraka zote kwa tume ya uchaguzi, Dkt Habineza amejibu maswali ya waandishi wa habari ambako amesema ana matumaini ya kushinda uchaguzi.

"Tuna matumaini zaidi ya asilimia 51 kwa sababu sisi ni chama kinachotaka mabadiliko. Kumbuka hiki ndicho chama pekee kilichopinga Rais Kagame kuongezewa muhula madarakani na tulipeleka madai yetu mahakamani japo hatukufanikiwa," amesema Dkt Habineza.

"Tume ya uchaguzi ilisema kwamba watu wapya zaidi ya milioni 1 wamewekwa katika daftari la wapiga kura kwa hiyo watu hao tuna matumaini kuwa wote watatuchagua."

Image caption Bw Mwenedata Gilbert, mgombea binafsi wa kiti cha urais akiwasili katika afisi za tume ya uchaguzi

Ameongeza kuwa chama chake cha Green kinajiimarisha mashinani licha ya vikwazo kadha wa kadha wa kadha, akinyooshea mkono viongozi wa mashinani kuwatatiza.

"Kama tulivyobainisha mwanzo, wakuu wa serikali za mitaa ndio tatizo kwa sababu wanawakilisha chama tawala mashinani.wanakuwa na wasi wasi kupokea vyama vingine wakishuku uhalali wa vyama hivyo,wamekuwa wakitutatiza."

Mgombea mwingine aliyewasilisha karatasi zake ni Mwenedata Gilbert ambaye katika uchaguzi huo anataka kuwania kama mgombea binafsi.

Wengine walioonyesha nia ya kugombea kiti cha urais ni mwanadada Diane Rwigara pamoja na Mpayimana Phillippe kama wagombea binafsi.

Upande wa chama tawala RPF kimekuwa katika mchakato wa kumteua mgombea wake ambapo rais Kagame anatarajiwa kuidhinishwa.

Tume ya uchaguzi ina hadi tarehe saba mwezi wa saba kutangaza rasmi wale watakaokuwa wamekubaliwa kugombea kiti cha urais kabla ya kampeni kutimua vumbi siku chache baadaye.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii