Trump anatumia nafasi yake kujinufaisha?

Rais Donald Trump anashutumiwa kutumia nafasi ya urais kujipatia faida zaidi Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Rais Donald Trump anashutumiwa kutumia nafasi ya urais kujipatia faida zaidi

Takriban wanachama 200 wa Democrats katika Bunge la Congress wameunganisha nguvu ili kufungua kesi dhidi ya Rais wa Marekani, Donald Trump kuhusu nyaraka za malipo kutoka serikali za nje kupitia biashara zake.

Trump anashutumiwa kukiuka kipengele cha katiba kuhusu malipo, kinachopiga marufuku kujipatia faida au fedha bila bunge kupitisha.

Wanachama hao wamesema idadi hii ni kubwa kuwahi kutokea kutaka kumshtaki Rais wa Marekani.

Maafisa wa Serikali na wafanyabiashara binafsi pia wanamfungulia mashtaka Trump kwa madai hayo hayo.

Lakini Ikulu ya Marekani imekana madai hayo.

Idara ya Sheria imekataa kuzungumzia madai hayo ya wabunge, lakini awali ilisema ni kinyume cha katiba kumshtaki Rais kama mtu binafsi.

Wabunge wamedai kuwa Trump hakutaka idhinisho la Congress kwa maipo yoyote yaliyopokelewa katika biashara zake Kutoka serikali za nje tangu alipoingia madarakani.

''Rais Trump ana mgongano wa maslahi katika nchi takriban 25, na inaonekana anatumia nafasi yake kujiongezea faida'' alieleza John Conyers, akinukuliwa na shirika la habari la Uingereza, Reuters.