Gazeti la Mawio lapigwa marufuku Tanzania

Uchimbaji wa madini nchini Tanzania
Image caption Uchimbaji wa madini nchini Tanzania

Serikali ya Tanzania imelipiga marufuku gazeti la kila wiki la Mawio kutochapishwa kwa kipindi cha miaka miwili baada ya kuwahusisha marais wa zamani Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete na kashfa ya madini nchini humo.

Waziri wa habari utamaduni na michezo Dkt Harrison Mwakyembe alilipiga marufuku gazeti hilo katika taarifa iliotolewa kwa vyombo vya habari na mkurugenzi wa huduma za habari Dkt Hassan Abbasi siku ya Alhamisi jioni.

Abbasi amesema kuwa marufuku hiyo inaanza mara moja.

Toleo la gazeti hilo la siku ya Jumatano liliweka picha za marais wa awali wa Tanzania pamoja na habari inayowahusisha na matatizo yanayokumba sekta ya madini nchini Tanzania.

''Nimelazimika kutumia uwezo niliopewa na sheria ya huduma za habari kulipiga marufuku gazeti la Mawio kutochapishwa kwa kipindi cha miezi 24'',ilisema barua hiyo kutoka kwa waziri iliokabidhiwa muhariri wa gazeti hilo.

Mbali na uchapishaji, gazeti hilo pia halitaruhusiwa kuendesha toleo lake la kidijitali ama hata katika mitandao ya kijamii.

Gazeti la Mawio limeshutumiwa kwa kupuuza agizo la serikali kutoripoti kuhusu marais hao wa zamani.

Siku ya Jumatano, rais Magufuli alivionya vyombo vya habari dhidi ya kuwahusisha Mkapa na Kikwete na ripoti za mzozo unaoendelea na kampuni kubwa ya uchimbaji madini ya Acacia.

Alitoa onyo hilo baada ya kufanya mazungumzo na mwenyekii wa Barrick Gold Profesa John Thornton katika Ikulu ya rais siku ya Juamatano.

''Vyombo vya habari vinafaa kusita kujiharibia sifa.Vimefanya kazi nzuri katika kutoa huduma katika taifa hili.Tuwawache wapumzike'', alisema rais.