Utafiti: Ziwa Tanganyika limo hatarini

Ziwa hilo ni tegemeo kubwa kwa watu takribani milioni 10 wanaoishi karibu nalo
Image caption Ziwa hilo ni tegemeo kubwa kwa watu takribani milioni 10 wanaoishi karibu nalo

Rasilimali za Ziwa Tanganyika zinatumiwa kwa kiwango ambacho si endelevu na kulifanya ziwa hilo ambalo ni la pili kwa ukubwa miongoni mwa maziwa yasiyo na maji yenye chumvi kuwa hatarini.

Mwezi wa kwanza mwaka huu, taasisi ya mazingira ya Ujerumani World Nature Fund ililiorodhesha Ziwa Tanganyika kuwa ziwa la mwaka lililo hatarini.

Uvuaji uliokithiri umesababisha upungufu mkubwa wa samaki.

Kwa mujibu wa baadhi ya utafiti, kiasi cha samaki ambacho mvuvi mmoja mmoja anakipata kwa siku kimepungua kwa takribani asilimia 80.

Baadhi ya wavuvi waliozungumza na BBC walithibitisha hali hii.

"Zamani tulikuwa tunavua samaki kati ya 300 na 500 kwa siku, ilikuwa inawezekana kabisa. Lakini hivi sasa mtu hupata samaki 30, 40, ukipata nyingi sana basi hawazidi 100," anasema Eliud Mheza ambaye amekuwa akivua samaki kwa takriban miaka 15.

Ziwa Tanganyika lina aina zaidi ya 1500 za samaki, wanyama na mimea ambazo asilimia 40 ya hizo hazipatikani mahali pengine popote ulimwenguni.

Ziwa hili, ambalo linapatikana katika nchi nne - Tanzania, Jamhuri ya Demkrasia ya Kongo, Burundi na Zambia - ni tegemeo kubwa la watu takribani milioni 10 wanaoishi pembezoni mwa ziwa hili.

Wanategemea ziwa hilo kwa usafiri, chakula, maji ya kunywa na uvuvi.

Image caption Idadi ya samaki imeanza kupungua na bei yao kupanda

Wanamazingira wanasema, ukataji miji na ukulima pembezoni mwa ziwa, umwagaji wa sumu kutoka viwandani na ile inayotumiwa na baadhi ya wavuvi katika uvuaji ni baadhi tu ya shughuli za kibinadamu zinazochangia kuhatarisha ziwa hili.

Lakini mabadiliko ya hali ya hewa ambayo yanasababisha kuchemka kwa maji ya ziwa hili na hivyo kuua baadhi ya chakula wanachotegemea samaki pia ni sababu kuu inayohatarisha Ziwa Tanganyika.

"Idadi ya samaki tunaoweza kuvua imeshuka sana ukilinganisha na siku za awali. Na idadi yao inapoongezeka, bei ndipo hushuka. Lakini sasa samaki ni wachache mno na bei yao imepanda sana, na kwetu wenye kiasi kidogo cha mtaji, inatuathiri sana," anasema Uwezo Yusufu, mchuuzi wa samaki.

Serikali za nchi zinazozungukwa na ziwa hili zimeunda taasisi iitwayo Mamlaka ya Ziwa Tanganyika ambayo inashughulikia ustawi wa Ziwa Tanganyika

"Serikali imeanzisha taasisi ambayo inafuatilia kwa karibu yanayojiri katika ziwa hili. Sehemu ya jukumu letu ni kuhakikisha watu wanaheshimu mipaka kwenye ziwa na kwamba hawajengi makao karibu sana na ziwa," anasema Rose Sallema, mtaalamu wa masuala ya ziwa katika Baraza la Usimamizi wa Mazingira Tanzania.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii