Mambo muhimu kuhusu sakata ya madini Tanzania

Rais John Magufuli akutana na Mwenyekito wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation,Prof John Thornton Haki miliki ya picha Google
Image caption Rais John Magufuli akutana na Mwenyekito wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation,Prof John Thornton

Rais wa Tanzania Dkt John Magufuli wiki hii alikutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation ambayo ni mmiliki mkubwa wa kampuni ya Acacia Mining Limited Prof John L Thornton.

Taarifa kutoka ikulu baada ya mkutano huo ilisema walikubaliana kuwa kampuni hiyo ipo tayari kufanya mazungumzo na Serikali ya Tanzania ili kulipa fedha ambazo Tanzania imezipoteza kutokana na kampuni hiyo kuendesha shughuli nchini Tanzania.

Baada ya Mazungumzo hayo Prof Thornton aidha alinukuliwa akisema kuwa kampuni yake ipo tayari kufanya mazungumzo na Tanzania yatakayozingatia maslahi ya pande zote mbili na pia ipo tayari kulipa fedha zote ambazo inapaswa kulipa kwa Tanzania.

Kwa upande wake Magufuli amesema Serikali inakaribisha mazungumzo hayo na itaunda jopo la wataalamu watakaofanya majadiliano na kampuni ya Barrick Jopo hilo litaundwa na wanasheria na maafisa wa serikali ili kufikia makubaliano ya kulipwa fedha zinazodaiwa na namna kampuni hiyo itakavyoendesha shughuli zake nchini maslahi ya pande zote mbili.

Rais Magufuli amesema pamoja na kukubali kulipa fedha zinazodaiwa Thornton amekubali kushirikiana na Tanzania kujenga mtambo wa kuchenjulia dhahabu (smelter) nchini Tanzania.

Lakini kampuni ya Acacia baadaye ilitoa taarifa fupi, ambapo ilisema katika mazungumzo hayo Barrick ilikubali kuanzisha mazungumzo na serikali ya Tanzania.

"Kwa kuwa mazungumzo hayajaanza, hakuna makubaliano yoyote yaliyoafikiwa, lakini mazungumzo yatatafuta suluhu ambayo itazingatia maslahi ya wadau wote," kampuni ya acacia ilisema Jumatano.

Kampuni ya Acacia Mining imeathirika?

Serikali ya Tanzania imeishutumu Acacia kwa kufanya kazi ya uchimbaji nchini Tanzania kinyume cha sheria na kusema kuwa makampuni ya uchimbaji madini yamekuwa yakikwepa kulipa kodi.

Kutokana na tuhuma hizo kutoka kwa serikali ya Tanzania, thamani ya hisa za kampuni ya Acacia ilishuka.

Uchunguzi ulioamriwa kufanyika mwezi Machi ulibaini kuwa Kampuni ya uchimbaji Acacia imekuwa ikifanya kazi kinyume cha sheria.

Mwenyekiti wa kamati ya wachumi na wanasheria Nehemiah Osoro iliyofanya uchunguzi huo alieleza. Kamati ilifanya uchunguzi kuhusu usafirishaji wa madini kwa kipindi cha miaka 19.

Hisa za Kampuni ya Acacia ambayo inamilikiwa na Barrick Gold Corparation zilianguka kwa kiasi cha asilimia 15.

Acacia imejitetea kuwa inafanya biashara zake kwa viwango vya juu na inafanya kazi kwa kufuata sheria za Tanzania ikiwemo kulipa kodi zote.

Haki miliki ya picha Ikulu Dar es Salaam
Image caption Rais Magufuli akihesabu makontena yenye mchanga wenye madini alipofanya ziara ya kushtukiza Machi

Tanzania imepoteza kiasi gani cha pesa?

Tanzania imepoteza takriban shilingi za kitanzania trilioni 188 (dola bilioni 84 za Marekani ) katika kipindi cha miaka 19 kati ya mwaka 1998 na mwaka 2017 kupitia usafirishaji wamakinikia ya dhahabu na shaba.

Hii ni kwa mujibu wa Ripoti ya Tume iliyoundwa mwezi Machi mwaka huu na Rais Magufuli.

Ripoti hii imekuja siku chache baada ya Ripoti ya kwanza iliyojikita kueleza kiasi cha madini na fedha ambazo Tanzania hupoteza kutokana na usafirishaji wa mchanga wenye madini.

Rais John Magufuli Alionyesha kukasirishwa na matokeo ya tume hiyo: ''Watu hawa hawana huruma, wanachukua dhahabu yote hii, lakini pia hawakulipa kodi,'' alieleza wakati wa kukabidhiwa ripoti hiyo, tukio lililoonyeshwa moja kwa moja kwa njia ya Televisheni.

Haki miliki ya picha Google
Image caption Rais wa Tanzania John Magufuli ametangaza kufanyia kazi mapendekezo yote ya kamati

Ripoti ya uchunguzi ilipendekeza nini?

Tume hiyo ilitoa mapendekezo 20, ambayo yote yalikubaliwa na Rais Magufuli. Miongoni mwa mapendekezo hayo ni kuwa:

  • kuendelea kuzuia usafirishwaji wa madini mpaka pale kodi za nyuma ziwe zimelipwa
  • Serikali idai kodi na mrahaba kutoka kwenye makampuni yote ya madini ambayo yamekwepa kulipa kodi na mrahaba stahiki kwa mujibu wa sheria.
  • Serikali ianzishe utaratibu utakaowezesha ujenzi wa kiwanda cha uchenjuaji wa makinikia yaani Smelter, ili kudhibiti upotevu wa mapato na kutengeneza mapato kwa watanzania.
  • Serikali ifanye uchunguzi na kuchukua hatua za kisheria, dhidi ya waliokua mawaziri,wanasheria wakuu wa serikali na manaibu wao, wakurugenzi wa idara za mikataba na makamishna wa madini, wanasheria wa Wizara ya madini na watumishi wengine wote waliohusika katika kuingia mikataba ya madini.

Tatizo ni nini?

Mtaalam wa uchumi kutoka chuo kikuu cha Kampala kampasi ya Dar es Salaam, Bravious Kahyoza, anasema ''mikataba ya madini ilivyo na sheria si tatizo pekee isipokuwa mifumo ya uchumi ilivyo inapohusishwa na uchumi wa dunia.

Hii si mara ya kwanza kuwepo kwa shutuma kuwa Barrick wanakwepa kodi.

Baada ya uchunguzi ilibainika kuwa ilitengeneza mazingira ya kukwepa kodi ya kiasi cha dola za marekani 41,250,426 kwa kipindi cha miaka minne mfululizo (2010-2013) fedha ambazo zilipaswa kulipwa kwa mamlaka ya mapato Tanzania, TRA.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii