Chama cha Macron chapata ushindi bungeni

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron Haki miliki ya picha EPA
Image caption Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron

Chama kinachoongozwa na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kimeibuka na ushindi wa viti vingi katika bunge la nchi hiyo, wiki kadhaa baada ya ushindi wake wa nafasi hiyo ya Urais.

Zikiwa karibu kura zote zimehesabiwa chama chake cha Republique en Merche, sambamba na washirika wao MoDem, walipata zaidi ya viti 300 kati ya viti 577 vya bunge la nchi hiyo.

Akilihutubia taifa Waziri mkuu wa Ufaransa, Edouard Phillippe, amesema amezielezea kura hizo zilizopigwa kuwa ni za matumaini.

Chama hicho kinachoongozwa na Rais Macron kiliundwa tu mwaka uliopita na nusu ya wagombea wake wana udhoefu mdogo wa masuala ya kisiasa huku wengine wakiwa hawana kabisa.

Matokeo hayo ya kura yamempa nguvu na uwezo Rais huyo mwenye umri wa miaka 39 wa kuwa na mamlaka ndani ya bunge la nchi hiyo na kuweza kuendelea na msimamo wake wa kufanya mabadiliko aliyoyanadi katika kampeni zake za uchaguzi.

Lakini hata hivyo, wapiga kura wachache walijitokeza katika awamu hiyo ya pili ya uchaguzi wa Bunge, kushinda ilivyo tarajiwa, huku rekodi yake ikikadiriwa kushuka kwa karibu asilimia 42, kulinganisha na miaka mitano iliyopita.

Katika uchaguzi huo, kiuongozi wa chama cha mrengo wa kulia Marine Le Pen, alipata ushindi kwa mara ya kwanza.